Wizara ya Elimu yatangaza ratiba ya usajili wa mitihani ya kitaifa ya 2026

0

Wizara ya Elimu imetangaza ratiba rasmi za usajili kwa ajili ya tathmini na mitihani ya kitaifa ya mwaka 2026, ikiwemo Tathmini ya Elimu ya Gredi ya 6 (KPSEA), Tathmini ya Elimu ya Gredi ya 9 (KJSEA) na Mtihani wa kitaifa wa Kidato cha 4 (KCSE).

Zoezi hilo litasimamiwa na Baraza la Mitihani la Kitaifa la Kenya (KNEC), ambalo lina jukumu la kuratibu mitihani yote ya kitaifa chini ya mfumo mpya wa elimu.

Akizungumza jijini Nairobi wakati wa uzinduzi wa msimu wa usajili, Waziri wa Elimu Julius Ogamba alisema serikali inaendelea kutekeleza mageuzi ya mfumo wa tathmini huku akitambua uungwaji mkono wa Rais William Ruto kwa sekta ya elimu.

Ogamba alieleza kuwa usajili wa KPSEA utaanza tarehe 16 Februari hadi 16 Machi 2026, huku usajili wa KJSEA ukifanyika kuanzia tarehe 2 Machi hadi 31 Machi 2026. Aidha, usajili wa watahiniwa wa KCSE utaanza tarehe 16 Februari na kuhitimishwa tarehe 31 Machi 2026.

Aidha amewataka wakuu wa shule kuhakikisha usajili unafanywa kwa usahihi na kwa wakati ili kuepusha matatizo yaliyoshuhudiwa katika miaka iliyopita.

Hata hivyo, Ogamba alieleza wasiwasi wake kuhusu makosa yanayofanywa na baadhi ya wakuu wa taasisi wakati wa zoezi la usajili, akibainisha kuwa makosa hayo yamesababisha baadhi ya wanafunzi kuathirika.

“Katika miaka ya nyuma, kumekuwa na visa vya wanafunzi kuathirika kwa sababu wakuu wa taasisi waliwasilisha taarifa zisizo sahihi, kwa mfano kuonyesha jinsia isiyo sahihi. Katika baadhi ya matukio, wanafunzi wengine hawakusajiliwa kabisa.” Ogamba alisema

Wizara imewahimiza wazazi na wanafunzi kufuatilia kwa karibu zoezi la usajili ili kuhakikisha taarifa zao ziko sahihi kabla ya shughuli ya usajili kutamatika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here