Rais aagiza wastaafu kupata mafao ndani ya siku kumi

0

Rais William Ruto ameagiza mageuzi katika mchakato wa malipo ya mafao ya kustaafu, akizielekeza taasisi zinazohusika na pensheni za watumishi wa umma kuhakikisha wanapokea mafao yao ndani ya siku 10 baada ya kustaafu.

Rais Ruto alisema agizo hilo linalenga kukomesha ucheleweshaji wa muda mrefu ambao kwa miaka mingi umewalazimu watumishi wa umma waliostaafu kufanya safari za mara kwa mara katika ofisi za serikali wakifuatilia malipo yao ya pensheni.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya walimu duniani yaliyofanyika, jijini Nairobi, Jumatatu tarehe 5 Oktoba, rais alisema muda huo mpya wa kushughulikia malipo hayo utaanza kutekelezwa kupitia mageuzi yanayolenga walimu, kabla ya kuenezwa katika utumishi mzima wa umma.

Alisema mfumo wa Taarifa za Usimamizi wa Pensheni, ulioanzishwa Julai 1, 2026 na Tume ya Huduma za Walimu (TSC) pamoja na hazina ya kitaifa, unatarajiwa kurahisisha ushughulikiaji wa madai ya mafao ya kustaafu.

“Mnamo Julai 1, 2026, TSC na Hazina ya Kitaifa zilianza kutekeleza mfumo wa taarifa za usimamizi wa pensheni ili kuharakisha malipo ya mafao ya kustaafu,” alisema rais Ruto.

Kwa mujibu wa kiongozi wa taifa, taasisi za serikali tayari zinaingiza taarifa za pensheni katika mfumo huo kwa maandalizi ya ushughulikiaji wa haraka wa madai huku taasisi zinazoshughulikia mafao ya kustaafu zikiwa zimetoa hakikisho kwamba lengo la siku 10 litaweza kufikiwa ndani ya miezi mitatu.

“Nimetoa maagizo ya wazi kwa Hazina ya Kitaifa ya Hifadhi ya Jamii kwamba kuanzia sasa, mafao yote ya kustaafu ya watumishi wetu wote wa umma lazima yawe tayari na yalipwe ndani ya siku kumi baada ya mfanyakazi kustaafu,” alisema.

Katika ujumbe uliowalenga zaidi walimu, rais alisema wastaafu hawapaswi kulazimika kusafiri kutoka ofisi moja hadi nyingine au kutafuta msaada wa kisiasa ili kupata fedha walizostahili kutokana na miaka yao ya utumishi.

“Tumesema kwamba mwalimu anapostaafu, hapaswi kuhangaika njiani akienda kutoka ofisi moja hadi nyingine, wala kuhangaika kumtafuta mbunge au mtu mwingine yeyote ili kumsaidia kupata mafao yake,” alisema.

Ahadi hiyo imetolewa huku kukiwa na malalamiko ya muda mrefu kuhusu ucheleweshaji katika kushughulikia malipo ya mafao ya kustaafu.

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here