Miili iliyopatikana mto Yala ilizikwa bila kudaiwa na familia  

0

Mamlaka huru ya uangalizi wa utendakazi wa polisi (IPOA) imefichua kuwa miili 15 kati ya 25 iliyopatikana katika mto Yala kati ya mwaka 2013 na 2025 ilizikwa bila kutambuliwa wala kudaiwa na jamaa zao.

Katika mkutano na wanahabari siku ya Jumanne Novemba 10, 2026, mamlaka hiyo ilisema kuwa ni miili 10 pekee iliyotambuliwa kupitia vipimo vya DNA na kukabidhiwa kwa familia kwa ajili ya mazishi, huku miili 15 iliyosalia ikizikwa bila kudaiwa.

Mwenyekiti wa IPOA, Dkt. Duncan Ojwang, amesema mamlaka hiyo ilichunguza visa vyote 25, kufanya vipimo vya DNA na kufanikiwa kulinganisha mabaki ya miili hiyo na familia 10 akiongeza kuwa sampuli za waathiriwa ambao hawajatambuliwa zimehifadhiwa kwa ajili ya uwezekano wa kutambuliwa siku zijazo.

IPOA imewasilisha matokeo ya uchunguzi wake kwa Jopo la wataalamu kuhusu fidia kwa waathiriwa wa ukiukaji wa haki za kibinadamu, kufuatia ombi la kutaka taarifa kuhusu mauaji yaliyotokea katika mto Yala.

Ojwang amesema IPOA iliweza kujibu ombi la jopo hilo kwa kutoa maelezo huru kuhusu yaliyowakumba waathiriwa wa mauaji hayo.

Mamlaka hiyo pia imesema imewasiliana na baadhi ya familia zilizoathirika, huku familia 10 zikiendelea kufuatilia madai ya fidia, ilhali kesi 15 zilizobaki zikishughulikiwa kupitia utaratibu tofauti ikiwataka watu wenye taarifa kuhusu waathiriwa hao kujitokeza.

Ripoti hiyo inatolewa wakati ambapo jopo la kushughulikia fidia linaelekea kukamilisha kazi yake ya kushughulikia madai yanayotokana na ukiukaji wa haki za kibinadamu wakati wa maandamano.

Mauaji ya mto Yala yalijulikana zaidi baada ya miili kadhaa kupatikana katika mto huo, kaunti ya Siaya, kwa kipindi cha miaka kadhaa, hali iliyozua wasiwasi kuhusu mauaji ya kiholela na kutoweshwa kwa watu kwa lazima.

Ugunduzi wa miili hiyo ulizua ghadhabu miongoni mwa wananchi na kuibua wito wa kufanyika kwa uchunguzi kuhusu mazingira yaliyopelekea vifo hivyo na uwezekano wa kuhusika kwa vyombo vya usalama.

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here