Kenya inafunga ubalozi wake mjini Bern, Nchini Uswisi, kuanzia Novemba 30, 2026, katika hatua ambayo serikali inasema inalenga kupanga upya uwakilishi wake wa kidiplomasia duniani kulingana na maslahi ya taifa.
Katibu katika Wizara ya Mambo ya Nje, Korir Sing’Oei, amesema hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa kufunga baadhi ya balozi na kufungua nyingine katika maeneo yanayopewa kipaumbele na serikali.
“Hii ni sehemu ya mpango unaoendelea wa kupanga upya uwakilishi wa kidiplomasia wa Kenya duniani, unaohusisha kufunga baadhi ya balozi na kufungua nyingine ili kuendeleza vipaumbele vyetu vya kimkakati kama nchi,” Sing’Oei amesema.
Hata hivyo, amewahakikishia Wakenya wanaoishi Uswisi kuwa hawatapoteza huduma za serikali kutokana na mabadiliko hayo.
“Wakenya wataendelea kupata huduma zilizo karibu nao licha ya mchakato huu wa kupanga upya uwakilishi wetu wa kidiplomasia,” ameongeza.
Katika notisi ya Novemba 9, ubalozi huo ulitangaza kuwa kitengo chake cha huduma za kibalozi kitafungwa Novemba 30, na kuwataka Wakenya wenye nyaraka zilizo tayari kuzichukua kabla ya tarehe hiyo.
Wale waliowasilisha maombi ya huduma za kibalozi kuanzia Novemba mosi watawasiliana nao kuhusu namna ya kupata nyaraka zao.
Serikali inatarajiwa kutoa maelezo zaidi kuhusu balozi nyingine zitakazoathiriwa na mpango huo pamoja na maeneo yatakayopata uwakilishi mpya wa kidiplomasia.









