Ukopaji Wa Serikali Unabana Biashara Na Fursa Za Ajira Nchini Serikali Yaonywa.

0
Mkurugenzi wa Benki ya Dunia Qimiao Fan, akizungumza katika Jukwaa la Uchumi la NCBA la mwaka 2026 jijini Nairobi, Novemba 3, 2026.
Mkurugenzi wa Benki ya Dunia Qimiao Fan, akizungumza katika Jukwaa la Uchumi la NCBA la mwaka 2026 jijini Nairobi, Novemba 3, 2026.

Benki ya Dunia imeonya kuwa kuendelea kwa serikali ya Kenya kukopa fedha katika soko la ndani kunabana upatikanaji wa mikopo kwa sekta binafsi, hali inayoweza kudhoofisha ukuaji wa biashara na juhudi za kubuni fursa za ajira nchini.

Mkurugenzi wa Benki ya Dunia, Dkt. Qimiao Fan, amesema ukopaji mkubwa wa serikali unaongeza ushindani wa upatikanaji wa fedha katika soko la ndani, huku biashara zikikabiliwa na changamoto ya kupata mikopo ya kugharamia shughuli zao na kupanua uwekezaji.

“Deni la taifa linafikia takriban asilimia 70 ya pato la taifa, huku zaidi ya nusu ya deni hilo likishikiliwa na wakopeshaji wa ndani, kuendelea kwa serikali kukopa katika soko la ndani kunaweza kubana mikopo inayotolewa kwa kampuni,” amesema Dkt. Fan.

Amesema biashara ndogo na za kati ndizo zinazoathirika zaidi na hali hiyo, licha ya kuwa zinachangia pakubwa katika kubuni fursa za ajira na kutegemea mikopo ya benki ili kuendesha na kupanua shughuli zao.

“Biashara ndogo na za kati ndizo zinazoathirika zaidi. Hata hivyo, ndizo zinazozalisha ajira nyingi katika uchumi na zinategemea pakubwa mikopo ya benki,” ameongeza.

Aidha Dkt. Fan ameelezea wasiwasi kuhusu kiwango cha chini cha uwekezaji wa sekta binafsi nchini, akisema hali hiyo imeendelea kwa takriban miongo miwili iliyopita.

Kwa mujibu wa Dkt. Fan, uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje ya nchi umekuwa wastani wa chini ya asilimia 0.5 ya pato la taifa tangu mwaka 2018, kiwango ambacho ni cha chini ikilinganishwa na wastani wa kati ya asilimia 1.5 na 2 katika mataifa yenye kipato cha chini na cha kati.

Amehusisha hali hiyo na gharama kubwa za kufanya biashara nchini, zikiwemo gharama za umeme na usafirishaji, pamoja na kutotabirika kwa sera za kodi na mazingira ya biashara.

“Kampuni zinakabiliwa na gharama kubwa, kuanzia umeme hadi usafirishaji, pamoja na mazingira ya biashara na kodi yasiyotabirika.

Hali hii inadhoofisha ushindani na uwezo wa kampuni kubuni fursa za ajira,” amesema Dkt. Fan.

Aidha, amesema changamoto za utawala na uwajibikaji zinaendelea kuathiri ufanisi wa sekta ya umma na imani ya wawekezaji, akitaja uwazi, na uwajibikaji kama nguzo muhimu katika kujenga mazingira yanayovutia uwekezaji.

Katika mapendekezo yake ya kuimarisha uchumi, Dkt. Fan ametoa wito kwa serikali kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma na usimamizi wa deni la taifa ili kupunguza shinikizo la ukopaji na kuongeza nafasi ya sekta binafsi kupata mikopo.

Pia amesisitiza umuhimu wa kuongeza uwazi na uwajibikaji serikalini, kupunguza gharama za kufanya biashara na kuweka mfumo wa usimamizi wa kodi ulio wazi na unaotabirika kwa wawekezaji.

Amesema Kenya inapaswa pia kuimarisha uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kutumia fursa za ukuaji wa uchumi wa kijani ili kupanua shughuli za kiuchumi na kupunguza athari za majanga yanayotokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Hata hivyo, Dkt. Fan amesema sekta ya kifedha nchini imeanza kuonyesha dalili za kuimarika, huku ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi ukiongezeka hadi asilimia 10.6 mwezi Septemba, kutoka takriban asilimia 5 mwaka mmoja uliopita.

Amesema viwango vya riba za mikopo vinaanza kupungua.

Pamoja na maendeleo hayo, amesisitiza umuhimu wa serikali kupunguza mahitaji yake ya ufadhili huku benki na wasimamizi wa sekta ya kifedha wakiendelea kulinda uthabiti wa mfumo wa benki na kuwezesha mikopo zaidi kuelekezwa kwa biashara binafsi, hususan biashara ndogo na za kati.

Akihitimisha hotuba yake, Dkt. Fan amesema Kenya imepiga hatua muhimu katika kudumisha uthabiti wa uchumi, ila bado inakabiliwa na changamoto za kifedha zinazohitaji mageuzi zaidi.

“Kenya inahitaji fedha zaidi kuelekezwa kwa kampuni na wajasiriamali wenye uwezo wa kuwekeza, kubuni mambo mapya, kukuza biashara na kubuni fursa za ajira,” amesema.

Amesema Benki ya Dunia itaendelea kuunga mkono Kenya kupitia uchambuzi wa kiuchumi, ufadhili na usaidizi wa kiufundi ili kuimarisha maendeleo ya muda mrefu nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here