DPP apendekeza adhadu ya kifo dhidi ya Mackenzie

0

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) ameiomba mahakama jijini Mombasa kumpa mhubiri tata, Paul Nthenge Mackenzie, adhabu ya kifo baada ya kumpata na hatia katika kesi ya mauaji ya halaiki ya Shakahola, ambapo watu 191, wakiwemo watoto 190, walifariki dunia kutokana na mafundisho potovu yaliyowashurutisha kufunga hadi kufa.

Akiwasilisha hoja za upande wa mashtaka kabla ya utoaji hukumu ulioratibiwa kufanyika tarehe 6 Novemba 2026, naibu mkurugenzi wa mashtaka ya umma, Jami Yamina, aliiambia mahakama kuwa adhabu ya kifo ndiyo inayofaa zaidi kwa Mackenzie, kutokana na uzito wa makosa aliyotenda na idadi kubwa ya watu waliopoteza maisha.

“Upande wa mashtaka unaunga mkono kutolewa kwa adhabu ya kifo dhidi ya Mackenzie, kwa kuzingatia hoja zake za kupunguziwa adhabu, majuto, kujutia makosa yake na uwezekano wa kurekebika,” Yamina aliwasilisha.

Mackenzie pamoja na washtakiwa wenzake 28 walipatikana na hatia ya makosa 191 ya mauaji yaliyotokana na vifo vilivyotokea katika msitu wa Shakahola, eneo bunge la Malindi, kaunti ya Kilifi, kati ya Januari 2021 na Septemba 2023.

DPP pia imeiomba mahakama kuwahukumu wengine 27 waliopatikana na hatia katika kesi hiyo kifungo cha maisha jela, ikisema kuwa adhabu hiyo inapaswa kuakisi uzito wa uhalifu waliotenda huku ikilinda umma dhidi ya madhara zaidi.

Yamina aliiambia mahakama kuwa utoaji wa hukumu unapaswa kuzingatia malengo kadhaa, yakiwemo kuzuia uhalifu wa siku zijazo, kulinda umma, kulaani vitendo vya uhalifu, kurejesha haki na kuwawezesha wahalifu kurekebika.

Upande wa mashtaka pia uliwasilisha mapendekezo kutoka kwa kituo cha kitaifa cha kukabiliana na ugaidi (NCTC), kikitaka wahusika kushiriki kwa hiari katika mipango ya kurekebishwa tabia na kukabiliana na mafundisho yenye misimamo mikali ili kuwawezesha kurejea katika jamii.

Iwapo mahakama itakosa kuridhia ombi lake, DPP imependekeza wahusika watolewe hukumu tofauti zinazotumikia moja baada ya nyingine, ikisema kuwa kila kifo kati ya vifo 191 kinawakilisha kosa tofauti la mauaji.

Katika kesi ya Enos Amanya Ngala, ambaye alikiri makosa yote 191 ya mauaji na kupatikana na hatia, upande wa mashtaka umeiomba mahakama kuzingatia masharti ya makubaliano yake ya kukiri mashtaka.

DPP imependekeza Ngala apewe mpango wa kurekebishwa kitabia akiwa gerezani kwa kipindi cha kati ya miezi 24 na 30, huku ripoti za mara kwa mara kuhusu maendeleo yake zikiwasilishwa ili kuongoza mapitio ya baadaye ya hukumu yake.

Jaji Diana Kavedza anatarajiwa kutoa hukumu dhidi ya wote 29 waliopatikana na hatia Novemba 6, 2026.

Kesi ya Shakahola ilitokana na kugunduliwa kwa makaburi ya halaiki na miili ya watu katika msitu wa Shakahola, ambapo wachunguzi walibaini kuwa mamia ya watu walikuwa wamefariki katika mazingira yaliyohusishwa na vuguvugu la kidini lililoongozwa na Mackenzie.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here