Jopo latetea uwazi katika mchakato wa fidia

0
Prof. Makau Mutua, mwenyekiti wa jopo la fidia kwa waathiriwa wa ukiukaji wa haki za kibinadamu.

Jopo la wataalamu kuhusu fidia kwa waathiriwa wa ukiukaji wa haki za kibinadamu limekana madai ya ufisadi na upendeleo katika mchako wa kuwafidia waathiriwa.

Jopo hilo linaloongozwa na Profesa Makau Mutua limesema hadi sasa limewafidia zaidi ya watu 700 waliojeruhiwa wakati wa maandamano, huku likishughulikia madai 236 ya watu walioaga dunia, zaidi ya madai 140 yanayohusiana na hasara za kiuchumi na madai 16 yanayohusu waathiriwa wa ukatili wa kingono.

Profesa Mutua ametoa ufafanuzi huo Jumanne tarehe 10 Novemba 2026, kufuatia wasiwasi kuhusu kuchelewa kwa mchakato wa utoaji fidia, pamoja na madai kwamba baadhi ya watu wanaojifanya kuwa wawakilishi wa jopo hilo wamekuwa wakiwataka waathiriwa kutoa fedha ili waweze kusaidiwa kupata fidia.

Mutua amewaonya waathiriwa na wananchi kwa jumla dhidi ya matapeli, watu wanaojifanya kuwa maafisa wa jopo hilo na madalali wanaotaka kujinufaisha kwa kuwaibia wanufaika.

Amesema jopo hilo linawaonya waathiriwa na umma dhidi ya watu wenye nia ovu, wakiwemo matapeli na madalali, wanaodai fedha kwa kisingizio cha kusaidia kurahisisha mchakato wa utoaji fidia.

Jopo sasa limeeleza mpango wa kuchapisha orodha ya watu ambao tayari wamepokea fidia, huku taarifa nyeti za kibinafsi zikifichwa ili kulinda utambulisho wao.

‘‘Uchapishaji wa taarifa hizo utaongozwa na sheria za ulinzi wa data, ambazo zinaitaka taasisi kulinda taarifa za waathiriwa na familia zao,’’ Alisema Prof. Mutua.

‘‘Kwa kuzingatia sheria hizo, jopo litachapisha taarifa zilizofanyiwa marekebisho kwa kuficha baadhi ya majina na maelezo ya waathiriwa, ili umma uweze kupata orodha kamili ya waliopokea fidia.’’ Aliongeza.

Amesisitiza kuwa kuficha utambulisho wa baadhi ya wanufaika ni muhimu kwa usalama wao, huku akithibitisha dhamira ya jopo hilo ya kuzingatia uwazi na uwajibikaji kwa umma.

Amesema baadhi ya familia za waathiriwa zimekubali kutembelewa na wajumbe wa jopo hilo pamoja na wanahabari, akitaja familia ya marehemu Rex Masai jijini Nairobi kama mfano.

Jopo hilo limepewa jukumu la kusimamia madai ya fidia kwa waathiriwa wa ukiukaji wa haki za kibinadamu, yakiwemo matukio yaliyotokana na maandamano na mikutano ya hadhara.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here