Wanaohusika na utekaji nyara kukabiliwa kisheria

0
CS Murkomen , IG Kanja and DCI Director Amin appears before the Senate on Ojwang Albert Death.
CS Murkomen , IG Kanja and DCI Director Amin appears before the Senate on Ojwang Albert Death.

Waziri wa Usalama na masuala ya ndani ya nchi, Kipchumba Murkomen, amepuuzilia mbali madai ya ongezeko la visa vya utekaji nyara nchini, akitetea serikali tawala kama iliyotimiza ahadi yake ya kukomesha mauaji ya kiholela yanayokiuka sheria pamoja na visa vya utekaji nyara.

Akifika mbele ya bunge la kitaifa Jumatano, Novemba 4, waziri Murkomen alisema kuwa takwimu zinaonyesha kupungua kwa visa vya utekaji nyara tangu serikali ya sasa ilipoingia mamlakani mwaka 2022.

Kwa upande mwingine, alidai kuwa wakati wa utawala uliotangulia, visa vya miili ya watu kupatikana katika mto Yala pamoja na watu kutoweka kwa lazima vilikuwa vimekithiri.

Waziri Murkomen aliongeza kuwa visa vyote vya hivi karibuni vya utekaji nyara vinaendelea kuchunguzwa na kwamba wote watakaopatikana kuhusika watachukuliwa hatua za kisheria.

Kuhusu suala la makundi ya wahuni, Murkomen alisema kuwa operesheni za kiusalama zimeimarishwa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 akiongeza kuwa washukiwa wa kupanga na kuchochea ghasia watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.

Murkomen alisema kuwa serikali imeimarisha operesheni za kiusalama kuelekea kipindi cha uchaguzi, huku ikiweka kipaumbele katika kupokea ratiba za mapema za mikutano ya kisiasa kutoka kwa viongozi wa serikali na upinzani ili kuwawezesha polisi kupanga mikakati ya kutosha ya usalama.

Matamshi ya Murkomen yanajiri wakati ambapo nchi imeshuhudia visa kadhaa vya utekaji nyara kinyume cha sheria na watu kutoweka kwa lazima, hali iliyozua hofu kubwa miongoni mwa wananchi, maandamano ya kupinga vitendo hivyo pamoja na kulaaniwa vikali na mashirika ya kutetea haki za binadamu.

Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu nchini (KNCHR) hivi majuzi ilirekodi visa vipya 46 vya watu kutoweka kwa lazima katika ripoti ya Mfumo wa Fidia kwa Waathiriwa (National Reparations Framework), iliyowasilishwa kwa rais mwezi Juni 2026.

Tume hiyo ilibainisha kuwa visa vingi vilihusisha waandamanaji waliokuwa wakizuiliwa katika maeneo yasiyojulikana bila mawasiliano na familia zao, pamoja na kuteswa.

Katika sehemu ya ripoti hiyo, tume ilieleza wasiwasi wake kuwa maswali kuhusu mahali walipo na hatima ya baadhi ya watu walioripotiwa kutoweka bado hayajajibiwa.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here