Seneta Veronica Maina amechukua nafasi ya naibu kiongozi wa upande wa walio wengi katika bunge la Seneti kutoka kwa seneta wa Nakuru, Tabitha Karanja, ambaye ameondolewa kutoka wadhifa huo.
Spika wa Seneti, Amason Kingi, Jumatano, Novemba 4, alitangaza rasmi mabadiliko hayo bungeni, akisema kuwa alikuwa amethibitisha nyaraka zilizowasilishwa na upande wa walio wengi kwa mujibu wa kanuni za kudumu za Seneti.
Maina alichaguliwa kushikilia wadhifa huo wakati wa mkutano uliofanyika Jumanne, Novemba 3, na hivyo kuchukua nafasi ya Karanja, aliyeondolewa kupitia azimio lililoungwa mkono na maseneta wa mrengo huo.
Katika taarifa yake kwa maseneta, Kingi alisema alikuwa amepokea barua ya tarehe 3 Novemba kutoka kwa kiranja wa upande wa walio wengi, David Wakoli, iliyomuarifu kuhusu mabadiliko katika uongozi.
Barua hiyo iliambatanishwa na kumbukumbu za mkutano pamoja na orodha iliyotiwa saini rasmi ya maseneta waliounga mkono azimio hilo.
Kingi alisema kuwa barua hiyo pamoja na kumbukumbu za mkutano zilionyesha kuwa lilipitishwa azimio la kumwondoa Seneta Tabitha Karanja kutoka wadhifa wa naibu kiongozi wa upande wa walio wengi katika Seneti, kwa mujibu wa kanuni ya kudumu ya 22(5) na 22(6).
Spika huyo alisema alikuwa amethibitisha nyaraka zilizowasilishwa na hivyo kutangaza rasmi kuwa Veronica Maina ndiye Naibu Kiongozi mpya wa upande wa walio wengi katika bunge la Seneti.
Mabadiliko hayo yanaanza kutekelezwa mara moja, huku Maina akitarajiwa kumsaidia seneta, Aaron Cheruiyot, kuratibu shughuli za muungano tawala ndani ya bunge hilo.
Kuondolewa kwa Keroche na kuchaguliwa kwa Maina kunaashiria mabadiliko katika uongozi wa muungano tawala katika Seneti, huku bunge hilo likiendelea na shughuli zake za kutunga sheria na kuisimamia serikali.









