
Serikali inalenga kupunguza malipo ya kila mwezi ya nyumba za bei nafuu kutoka takribani shilingi elfu 45 hadi elfu 15.
Mwenyekiti wa Baraza la Washauri wa Rais kuhusu Masuala ya Uchumi, Dkt. David Ndii, anasema mpango huo unalenga kuondoa vikwazo vya kifedha vinavyozuia wananchi wengi kumiliki nyumba katika maeneo ya mijini.
Ndii anasema serikali inatarajia kupunguza gharama hizo kupitia utoaji wa ardhi ya umma, uwekezaji katika miundombinu na mifumo nafuu ya ufadhili.
“Kwa kutoa ardhi ya umma na kugharamia miundombinu ya msingi, pamoja na kuweka mifumo nafuu ya ufadhili, tunaweza kupunguza malipo hayo kutoka shilingi elfu 45 hadi elfu 15,” amesema Ndii.
Ameongeza kuwa kupunguza malipo hayo kunaweza kuongeza idadi ya familia zinazoweza kumiliki nyumba mijini kutoka takribani laki mbili hadi milioni mbili.
“Ukishusha malipo hayo hadi shilingi elfu 15, hata watu wanaopata kipato cha shilingi elfu 45 kwa mwezi wataweza kuingia katika mfumo wa umiliki wa nyumba,” amesema.
Ndii amefafanua kuwa mpango wa nyumba za bei nafuu hauhusu kuboresha makazi duni pekee, bali unalenga pia soko pana la nyumba za mijini, kupitia ujenzi wa nyumba za bei nafuu na za kibiashara katika miradi hiyo.
Katika juhudi za kufadhili miradi mikubwa ya maendeleo, serikali pia inaendeleza mpango wa Mfuko wa Kitaifa wa Miundombinu (National Infrastructure Fund), unaolenga kuvutia uwekezaji kutoka sekta binafsi.
Ndii amesema serikali inalenga kufunga mikataba ya uwekezaji yenye thamani ya takribani dola bilioni 10 kufikia robo ya kwanza ya mwaka 2027, ikihusisha miradi ya viwanja vya ndege, barabara kuu, umeme na reli.
“Kati ya sasa na robo ya kwanza ya mwaka ujao, tunatarajia kufunga mikataba ya uwekezaji yenye thamani ya takribani dola bilioni 10,” amesema Ndii.
Ameongeza kuwa lengo la muda mrefu ni kufadhili miradi ya miundombinu yenye thamani ya dola bilioni 40, sawa na takribani shilingi trilioni tano.








