Mariga Apinga Kuondolewa FKF, Aitaka Fifa Kuchunguza Mkutano Wa Meru.

0

Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka nchini (FKF), Mcdonald Mariga, amepinga uamuzi wa kuwaondoa maafisa saba wa Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC), akitaka FIFA, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Msajili wa Michezo kuchunguza uhalali wa mkutano uliofanyika Meru Novemba 7, 2026.

Katika taarifa yake Jumatatu Novemba 9 2026, Mariga amesema maamuzi ya mkutano huo maalum yalikiuka katiba ya FKF na hivyo maafisa walioathirika wataendelea kushikilia nyadhifa zao kwa kuwa hawatambui uamuzi huo.

Mariga anadai kuwa yeye pamoja na maafisa wengine sita wa NEC na wajumbe 32 wa kongamano la FKF waliokuwa wameidhinishwa walizuiwa kuingia katika ukumbi wa mkutano, hatua aliyosema iliwanyima nafasi ya kushiriki katika maamuzi.

Aidha, amepinga utaratibu uliotumika kuwaondoa maafisa hao, akirejelea Kifungu cha 41(4) na (5) cha katiba ya FKF, kinachowapa maafisa wanaokabiliwa na hatua za kinidhamu haki ya kusikilizwa na kuhitaji maamuzi ya kuwaondoa yafanywe kupitia kura ya siri.

Hata hivyo, Mariga anasema badala ya kura ya siri, azimio la kuwaondoa maafisa hao lilipitishwa kwa makubaliano ya pamoja.

“Kifungu cha 41(5) kinaeleza wazi kuwa hoja ya kumwondoa afisa lazima iamuliwe kupitia kura ya siri. Hili ni sharti la lazima la kikatiba, si utaratibu wa hiari.” Amesema.

Mariga amezitaka FIFA, CAF na Msajili wa Michezo kuchunguza wajumbe walioshiriki mkutano, rekodi za mahudhurio, idadi ya wajumbe waliohitajika ili mkutano uwe halali pamoja na utaratibu wa upigaji kura.

Aidha, amedai kulikuwa na watu walioshiriki kama wajumbe bila kuwa na idhini halali ya kuwawakilisha wengine.

Mkutano huo maalum uliofanyika katika Hoteli ya Three Steers mjini Meru ulipitisha azimio la kuwaondoa maafisa saba wa NEC, akiwemo Mariga, kwa kura 65 kati ya wajumbe 66 waliohudhuria.

Maafisa wengine walioondolewa ni Robert Macharia, Gabriel Mugendi, Dan Shikanda, Caleb Collins, Bernard Lagat na Violet Kirubo.

Hata hivyo, Mariga amesisitiza kuwa hatua yao si kulinda nyadhifa zao binafsi, bali ni kutetea utawala bora na kufuatwa kwa katiba ndani ya shirikisho hilo.

“Hatutatishwa, kunyamazishwa wala kulazimishwa kuachana na wajibu wetu kwa soka la Kenya.” Ameongeza.

Maafisa hao wamesema wanahifadhi haki ya kupinga maamuzi ya mkutano huo kupitia njia za kikatiba na kisheria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here