Wakenya sita wamewasilisha kesi katika Mahakama Kuu ya Milimani wakitaka serikali kufichua makubaliano ya kifedha kuhusu mechi ya kirafiki kati ya Timu ya Bayern Munich ya Ujerumani na Ajax ya Uholanzi, inayotarajiwa kuchezwa katika uwanja wa Talanta Januari 5, 2027.
Katika kesi hiyo, sita hao wanaitaka serikali kueleza iwapo fedha za walipa kodi zitatumika kugharamia mechi hiyo, ikiwemo ada za timu kushiriki, usafiri, malazi, usalama, bima na gharama nyingine za maandalizi.
Pia wanaitaka mahakama kuzuia serikali kutenga, kutoa au kutumia fedha za umma kwa ajili ya mechi hiyo hadi ithibitishwe kuwa matumizi hayo yanazingatia Katiba na sheria za fedha.
Kesi hiyo imewasilishwa kufuatia tangazo la Rais William Ruto la Oktoba 28, 2026, kuhusu mechi hiyo.
“Mechi hii itaandaliwa kupitia ushirikiano na kampuni binafsi pamoja na mfumo wa kibiashara unaojitegemea.” Rais alisema
Katika kiapo chake, mlalamishi wa kwanza, Erick Sayialel Mankuyu, amesema kauli ya Rais kuhusu ufadhili wa kibiashara haujaondoa wasiwasi kuhusu uwezekano wa walipa kodi kubebeshwa gharama za tukio hilo.
“Hatupingi maendeleo ya michezo, ushirikiano wa kimataifa katika michezo au kuandaliwa kwa mechi za kimataifa nchini Kenya.” Mankuyu amesema.
“Wasiwasi wetu ni iwapo mipango ya kifedha inayopendekezwa inahakikisha thamani ya fedha, matumizi halali, uwazi na manufaa yanayoweza kuonekana.” Ameongeza
Walalamishi hao wanataka Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dorcas Oduor, Waziri wa Michezo Salim Mvurya na Waziri wa Fedha John Mbadi pamoja na shirika la Sports Kenya kufichua utambulisho wa wadhamini, michango yao na mikataba inayosimamia maandalizi ya mechi hiyo.
Pia wanataka nyaraka hizo ziwasilishwe ndani ya siku saba.
Wamerejelea Ibara ya 35 ya Katiba inayohakikisha haki ya kupata taarifa kutoka kwa serikali, pamoja na Ibara ya 201 inayotaka uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma.
Pia wameomba mahakama itangaze ombi hilo kuwa la dharura na kutoa amri za muda za kuzuia matumizi ya fedha za umma, huku ikitaka nyaraka zote za kifedha, mikataba ya udhamini na ununuzi zihifadhiwe hadi kesi hiyo itakaposikilizwa na kuamuliwa.









