Aliyekuwa Kamishna Wa Mkoa Wa Nairobi Asukumwa Miaka Mitatu Gerezani.

0
Aliyekuwa Kamishna wa Mkoa wa Nairobi, Davis Nathan Chelogoi katika Mahakama ya Milimani
Aliyekuwa Kamishna wa Mkoa wa Nairobi, Davis Nathan Chelogoi katika Mahakama ya Milimani

Aliyekuwa Kamishna wa Mkoa wa Nairobi, Davis Nathan Chelogoi, amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela bila faini baada ya kupatikana na hatia katika kesi ya ulaghai wa ardhi inayohusisha mali yenye thamani ya takriban shilingi bilioni 1.3 inayohusu kipande cha ardhi chenye utata eneo la Lower Kabete.

Chelogoi mwenye umri wa miaka 76, alipatikana na hatia katika makosa sita.

Mahakama iliamuru vifungo hivyo vitumikie kwa wakati mmoja, hivyo adhabu yake ya mwisho kuwa miaka mitatu gerezani.

Wakati wa kuomba apunguziwe adhabu, wakili wake, David Kinyanjui, aliiomba mahakama izingatie umri wake, hali yake ya kiafya na utumishi wake wa takriban miaka 40 serikalini.

Aidha ameeleza kuwa Chelogoi ni mjane anayekabiliwa na matatizo ya moyo na changamoto nyingine za kiafya zinazohusiana na umri wake.

“Kwa kuzingatia makosa anayokabiliwa nayo pamoja na umri wake, ninaamini mahakama itafikia uamuzi wa kumpa adhabu isiyohusisha kifungo gerezani.” Amesema Wakili Kinyanjui.

Kinyanjui ameongeza kuwa mteja wake alishirikiana na mahakama tangu mwanzo wa kesi na hakukosa kikao chochote.

“Mshtakiwa ameshirikiana na mahakama tangu mwanzo. Hakukosa siku yoyote ya kusikilizwa kwa kesi. Yeye ni raia anayeheshimu sheria.” Amesema Wakili Kinyanjui.

Hata hivyo, upande wa mashtaka ulipinga ombi la adhabu isiyohusisha kifungo gerezani, ukisema mahakama inapaswa pia kuzingatia madhara waliyopata walalamikaji.

“Msisitizo mkubwa umewekwa kwa mshtakiwa, lakini tungependa pia kuieleza mahakama kuwa waathiriwa nao ni watu wenye umri mkubwa. Wamevumilia mchakato huu wote wa kesi tangu mwaka 2023. Haki inapaswa kutendeka kwa pande zote.” Upande wa Mashtaka umeeleza.

Mahakama ilipokea rasmi ripoti ya tathmini ya athari kwa waathiriwa na kuufahamisha upande wa utetezi kuwa una haki ya kukata rufaa ndani ya siku 14 tangu kutolewa kwa hukumu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here