Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Jaji Mstaafu Paul Kihara Kariuki amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 72.
Kifo chake kimethibitishwa na Jaji Mkuu Martha Koome, kupitia taarifa iliyotolewa Jumanne, tarehe 3 Novemba 2026.
Katika taarifa hiyo, Koome amesema amepokea habari za kifo cha Kihara kwa masikitiko makubwa, amemmiminia sifa tele kimtaja kuwa alikuwa mwanasheria mahiri.
“Jaji Kihara Kariuki alikuwa mwanasheria mahiri, kiongozi wa kipekee katika mahakama na mtumishi wa umma aliyejitolea, ambaye mchango wake katika usimamizi wa haki na maendeleo ya taasisi za kisheria nchini Kenya utaendelea kuwa sehemu muhimu ya historia ya taasisi zetu.” Koome amesema.
“Tunapoomboleza kifo chake, pia tunaangazia maisha yake yaliyotolewa kwa ajili ya sheria, utumishi wa umma na kuimarisha taasisi zinazolinda utawala wa sheria.” Ameongeza.
Kihara aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu mwaka 2003, kabla ya kupandishwa cheo na kujiunga na Mahakama ya Rufaa.
Baadaye alichaguliwa na majaji wenzake kuwa Rais wa kwanza wa Mahakama ya Rufaa chini ya Katiba ya mwaka 2010, akihudumu katika nafasi hiyo kuanzia mwaka 2013 hadi 2018.
Katika kipindi chake, aliongoza mageuzi yaliyolenga kuboresha ufanisi na upatikanaji wa huduma za mahakama, yakiwemo kusambaza shughuli za Mahakama ya Rufaa katika maeneo mbalimbali nchini.
Pia alihudumu kama Mkurugenzi mwanzilishi wa Taasisi ya Mafunzo ya Mahakama.
Koome amesema uongozi wa Marehemu uliweka msingi wa mfumo rasmi wa mafunzo na maendeleo ya kitaaluma kwa majaji, maafisa wa mahakama na wafanyakazi wengine wa idara hiyo.
Baada ya kuhudumu katika Mahakama ya Rufaa, Kihara aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwaka 2018, nafasi aliyoishikilia hadi mwaka 2022, akiwa mshauri mkuu wa kisheria wa Serikali.









