Rais Aongoza Taifa Kumwomboleza Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu.

0
Rais William Ruto Amwomboleza Marehemu Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Paul Kihara.

 

Rais William Ruto ameliongoza taifa kuomboleza kifo cha aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Rais mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Paul Kihara Kariuki, aliyefariki Jumanne tarehe 3 Novemba 2026 akiwa na umri wa miaka 72.

Katika taarifa, Rais Ruto amemtaja Kariuki kuwa mwanasheria mahiri na mtumishi wa umma aliyejitolea.

“Tutamkumbuka Jaji Kihara kama mwanasheria mahiri na mtumishi wa umma aliyejitolea, aliyetoa mchango mkubwa katika maendeleo na uimarishaji wa taasisi za sheria na mahakama nchini.” Ruto amesema.

Rais pia amesisitiza mchango wa Kariuki katika kuanzishwa kwa Taasisi ya Mafunzo ya Mahakama, ambako alihudumu kama mkurugenzi wa kwanza na kusaidia kuimarisha mafunzo ya kitaaluma kwa majaji na maafisa wa mahakama.

Kwa upande wake, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta pia ameomboleza Kariuki, akimtaja kuwa jaji mashuhuri na mtumishi wa umma aliyejitolea, ambaye utumishi wake wa muda mrefu kama Mwanasheria Mkuu na Rais wa Mahakama ya Rufaa uliacha alama ya kudumu katika taasisi za mahakama na utumishi wa umma nchini.

“Jaji Paul Kihara alikuwa jaji mashuhuri na mtumishi wa umma aliyejitolea, ambaye taaluma yake ndefu na yenye mafanikio kama Mwanasheria Mkuu na Rais wa Mahakama ya Rufaa iliacha alama isiyofutika katika taasisi za mahakama na za umma nchini.” Uhuru amesema.

Uhuru pia ametuma risala za rambirambi kwa familia, marafiki na jamaaa akiwaombea nguvu na faraja katika kipindi hiki kigumu.

Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula amesema Kariuki alijitolea maisha yake kulitumikia taifa na kuendeleza utawala wa sheria.

“Kifo chake ni pigo kubwa kwa taaluma ya sheria na taifa letu. Tumempoteza mwenzetu aliyeheshimika, ambaye urithi wake wa uadilifu, weledi na utumishi utakumbukwa.” Wetang’ula amesema.

Jaji Mkuu Martha Koome, ambaye alitangaza kifo chake Jumanne, amemtaja Kariuki kuwa kiongozi wa mahakama aliyekuwa na mchango wa kudumu katika historia ya taasisi za sheria nchini.

Kariuki alikuwa na tajriba ya zaidi ya miaka 40 katika taaluma ya sheria.

Aliteuliwa kuwa jaji wa Mahakama Kuu mwaka 2003 kabla ya kujiunga na Mahakama ya Rufaa.

Kati ya mwaka 2013 na 2018, alihudumu kama Rais wa kwanza wa Mahakama ya Rufaa kufuatia kuchaguliwa na majaji wenzake chini ya Katiba ya mwaka 2010.

Katika kipindi hicho, aliongoza mageuzi yaliyolenga kuboresha upatikanaji wa haki, ikiwemo kusambaza huduma za Mahakama ya Rufaa katika maeneo ya Malindi, Kisumu na Nyeri.

Mwaka 2018, aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa saba wa Kenya, nafasi aliyohudumu hadi Oktoba 2022.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here