Wizara ya Afya, imetangaza kuwa Kenya imefanikiwa kuwafuatilia watu wote 135 waliokuwa wametangamana na mgonjwa wa kwanza wa Ebola nchini, huku serikali ikiimarisha juhudi za kudhibiti mlipuko wa ugonjwa huo.
Akifika mbele ya bunge la kitaifa Jumanne, tarehe 3 Novemba 2026, waziri wa Afya Aden Duale alisema kuwa serikali imefanikiwa kutekeleza zoezi la kuwafuatilia watu wote waliokutana na mgonjwa huyo kwa asilimia 100.
Waziri Duale alifichua kuwa miongoni mwa watu waliofikiwa ni abiria na wahudumu wa ndege waliokuwa safarini pamoja na mgonjwa wa kwanza, wafanyakazi wa uwanja wa ndege, maafisa wa uhamiaji na forodha, wahudumu wa afya pamoja na wanafamilia waliokutana na mgonjwa huyo.
“Tumefanikisha ufuatiliaji wa watu wote kwa asilimia 100. Kenya ndiyo nchi pekee iliyofanikiwa kufanya hivyo. Kenya inapaswa kupongezwa na kusherehekewa kimataifa badala ya kuwekewa vikwazo vya usafiri,” Duale aliiambia kamati ya bunge.
Kwa mujibu wa Duale, wahudumu 45 wa afya ni miongoni mwa watu 135 waliotambuliwa kutangamana na mgonjwa huyo na ambao kwa sasa wamewekwa karantini.
Duale alifichua zaidi kuwa mamlaka za Kenya zimefanikiwa kumpata mtu aliyekuwa amesafiri pamoja na mgonjwa huyo wa kwanza lakini baadaye akaendelea na safari hadi Mogadishu nchini Somalia.
Alisema serikali pia ilikuwa imezitaarifu nchi ambazo mgonjwa huyo na watu wengine waliokuwa na mawasiliano naye walipitia katika safari zao, kwa mujibu wa kanuni za kimataifa za afya.
Waziri huyo alitetea namna Kenya ilivyoshughulikia mlipuko huo, akisisitiza kuwa mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa, kuwafuatilia watu waliokutana na wagonjwa pamoja na hatua za kudhibiti maambukizi imekuwa na ufanisi katika kuzuia kuenea kwa virusi hivyo.
Pia alikosoa vikwazo vya usafiri vilivyowekwa na Saudi Arabia kufuatia mlipuko huo, akisema kuwa hatua hizo haziambatani na mapendekezo ya kimataifa kuhusu afya ya umma.
Duale alifichua kuwa wizara ya Mambo ya Nje ilikuwa imewasilisha rasmi malalamishi yake kwa mamlaka za Saudi Arabia na kuwa mazungumzo ya kidiplomasia yalikuwa yakiendelea ili vikwazo hivyo vifanyiwe mapitio.
Alisema Shirika la Afya Duniani (WHO), Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) pamoja na ofisi yake walikuwa wamewasiliana na mamlaka za Saudi Arabia kuhusu suala hilo.
“WHO imezungumza kwa niaba yetu na serikali ya Saudi Arabia. Africa CDC pia imezungumza kwa niaba yetu. Mimi mwenyewe nimezungumza na waziri wa Afya wa Ufalme wa Saudi Arabia,” alisema.
Kwa mujibu wa Duale, Saudi Arabia ilikuwa ikipitia upya ushauri wake kuhusu safari, huku serikali ya Kenya ikiwa na matumaini ya kupata matokeo mazuri.
Wakati wa kikao cha kamati hiyo, Duale pia alitetea uamuzi wa serikali kuanzisha kanuni za kuzuia na kudhibiti Ebola bila kutekeleza utaratibu wa kawaida wa ushirikishwaji wa umma.
“Tunakabiliana na tishio kubwa kwa afya ya umma, kwa hivyo hatuna muda wa kutosha wa kuzunguka, kuchapisha matangazo kwenye magazeti na kuwauliza watu maoni yao kuhusu namna ya kushughulikia suala hili. Sheria ya Afya ya Umma, kupitia Kifungu cha 5A, inanipa mimi kama waziri wa Afya mamlaka ya kuwasilisha kanuni hizo,” alisema.
Serikali imesisitiza kuwa hatua za ufuatiliaji na udhibiti wa ugonjwa huo zinaendelea kutekelezwa huku mamlaka za afya zikiendelea kufuatilia hali ya mlipuko huo.









