Kenya Yathibitisha Kisa cha Tisa Cha Ebola.

0

Kenya imethibitisha kisa kingine cha Ebola, na kufikisha jumla ya visa vilivyothibitishwa kuwa tisa, kikiwemo kisa cha kwanza cha mgonjwa aliyefariki kutokana na ugonjwa huo.

Mkurugenzi Mkuu wa Afya nchini, Dkt. Patrick Amoth amesema kisa cha tisa kinamhusu mwanamume mwenye umri wa miaka 24 ambaye ni jamaa wa karibu wa mgonjwa wa kwanza.

Kwa mujibu wa Amoth, mwanamume huyo alikuwa tayari ametengwa kwa kuwa alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wamekutana na mgonjwa wa kwanza.

“Kisa kipya ni mtu anayejulikana kuwa na mawasiliano na mgonjwa wa kwanza na alikuwa tayari karantini alipoanza kuugua. Visa vyote tisa vinatokana na kundi moja la maambukizi, na kufikia sasa hakuna ushahidi wa maambukizi kusambaa nje ya kundi hilo,” imesema wizara hiyo.

Wizara ya Afya imeongeza kuwa wagonjwa wanane walionusurika wanaendelea kupata nafuu na wako katika hali njema huku wakipatiwa matibabu na kufuatiliwa kwa karibu na wahudumu wa afya.

Pia imeeleza kuwa imepokea dozi 500 za dawa za kusaidia matibabu ya wagonjwa waliothibitishwa kuwa na Ebola.

Wakati uo huo, juhudi za kufuatilia watu waliokuwa na mawasiliano na wagonjwa zinaendelea.

Kufikia Jumanne Oktoba tarehe 20 2026, watu 134 kati ya 135 waliotambuliwa kuwa na mawasiliano na wagonjwa walikuwa wamepatikana na kuwekwa kwenye karantini ikiashiria asilimia 99.3.

Amoth amesema kuongezeka kwa idadi ya watu wanaofuatiliwa kunatokana na kutambuliwa kwa watu wengine walioweza kuwa na mawasiliano na wagonjwa wapya waliothibitishwa.

“Kila kisa kipya kinapothibitishwa, watu waliokuwa na mawasiliano na mgonjwa huongezwa kwenye orodha ya wanaofuatiliwa, na hilo ndilo linaloeleza kuongezeka kwa idadi ya watu wanaofuatiliwa,” amesema Amoth.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here