Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Kuenea kwa Magonjwa Africa CDC kimeahidi msaada wa takriban dola milioni 1.5 kusaidia Kenya kudhibiti mlipuko wa Ebola, ikiwemo kutuma wataalamu wa afya na kutoa vifaa vya uchunguzi.
Hatua hiyo ilitangazwa baada ya Waziri wa Afya Aden Duale kukutana na Mkurugenzi Mkuu wa Africa CDC, Dkt. Jean Kaseya Jumanne, Oktoba 27, 2026 na kumweleza kuhusu juhudi za serikali za kukabiliana na mlipuko huo.
“Tunapongeza uongozi thabiti wa kisiasa wa serikali ya Kenya, uhamasishaji wa haraka wa rasilimali na hatua madhubuti za kudhibiti mlipuko huo, ugunduzi wa mapema, hatua za haraka, ufuatiliaji madhubuti na uratibu wa kitaifa ni muhimu katika kupunguza maambukizi na kulinda maisha.” Kituo hicho Kimesema.
Msaada huo unajumuisha wataalamu 10 wa afya ya umma kutoka Afrika, vifaa vya kisasa vyenye thamani ya takriban dola 350,000, vifaa vya uchunguzi wa maabara na msaada wa kufuatilia waliokutana na wagonjwa, pamoja na kusimamia matibabu na kutoa elimu kwa jamii.
“Juhudi za Kenya za kudhibiti mlipuko huo ni muhimu si tu kwa kulinda wananchi wake, bali pia katika kupunguza hatari ya maambukizi kuenea katika nchi nyingine.”
Taasisi hiyo pia imesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika kudhibiti milipuko wa Ebola
“Hakuna nchi inayoweza kukabiliana na dharura ya afya ya umma peke yake,” Imesema.
Wakati uo huo, Africa CDC imeitisha mkutano wa dharura wa mawaziri wa afya wa Afrika utakaofanyika Oktoba 28, 2026.
Mkutano huo ukilenga kutathmini hali ya Ebola, kuimarisha uratibu na kukubaliana kuhusu hatua za haraka za kukabiliana na mlipuko huo.









