Jopo la wataalamu la kushughulikia fidia kwa waathiriwa wa ukiukaji wa haki za binadamu limeweka Novemba 14, 2026, kuwa tarehe ya mwisho ya kupokea madai mapya kutoka kwa waathiriwa wanaotafuta fidia, wakiwemo walioathiriwa na maandamano.
Katika tangazo la umma, lililotolewa Jumanne tarehe 27 Oktoba 2026, jopo hilo limewahimiza waathiriwa ambao bado hawajawasilisha madai yao kufanya hivyo kabla ya tarehe hiyo ili kuhakikisha kuwa maombi yao yanazingatiwa katika mpango wa fidia.
Jopo hilo, linaloongozwa na Profesa Makau Mutua, limesema madai yote yatakayopokelewa kabla ya muda wa mwisho, yakiwemo yale ambayo tayari yamewasilishwa, yatafanyiwa uhakiki na uthibitishaji kabla ya maamuzi kufanywa.
“Tumejizatiti kuhakikisha kuwa kila mwathiriwa anayestahili anashughulikiwa kwa haki na kwa heshima,” alisema Mutua.
Jopo hilo limesema watakaowasilisha maombi watajulishwa kuhusu maamuzi ya maombi yao kwa wakati unaofaa, huku likiwataka kuwa na subira wakati mchakato wa uhakiki unapoendelea.
Limeongeza kuwa linaendelea kupiga hatua katika kushughulikia maombi na kutoa fidia kwa waathiriwa katika makundi mbalimbali ya madhara, yakiwemo vifo, majeraha ya mwili, ukatili wa kingono, hasara za kiuchumi na ukiukaji mwingine unaotambuliwa.
Jopo hilo limesema litaendelea kutoa taarifa za mara kwa mara kwa umma kuhusu hali ya utekelezaji wa mpango wa fidia, ikiwa ni sehemu ya dhamira yake ya kuimarisha uwajibikaji na uwazi.
Pia limethibitisha tena dhamira yake ya kushirikiana moja kwa moja na waathiriwa na wanufaika ili kushughulikia wasiwasi wao, kufafanua hali ya madai yao na kuhakikisha wanatendewa kwa heshima katika kipindi chote cha mchakato.
Waathiriwa wanaohitaji maelezo zaidi kuhusu mpango wa fidia wameelekezwa kutembelea ofisi za jopo hilo zilizopo kwenye jumba la mikutano la kimataifa (KICC), jijini Nairobi.
Jopo hili lilianzishwa na serikali kwa lengo la kurahisisha utambuzi, uhakiki na utoaji wa fidia kwa waathiriwa wa ukiukaji wa haki za binadamu, ikiwemo ile iliyotokana na maandamano na mikusanyiko ya umma.
Jukumu lake ni kutathmini madai kutoka kwa watu binafsi na familia zilizoathiriwa, kubaini wanaostahili kupata fidia na kupendekeza hatua zinazofaa za kurekebisha madhara waliyopata, kama vile vifo, majeraha, ukatili wa kingono na hasara za kiuchumi kama sehemu ya juhudi za kuimarisha uwajibikaji, haki na ulinzi wa utu wa waathiriwa.









