Chama cha Wanasheria nchini (LSK) kimeongeza shinikizo kwa vyombo vya usalama kuhusu kutoweka kwa wakili wa Nairobi, Abshir Ahmedsadak Abdi, kikisisitiza kuwa hakitakata tamaa hadi atakapopatikana salama na kuunganishwa tena na familia yake.
Abdi alitoweka katika mazingira ya kutatanisha alfajiri ya Novemba 1, 2026, hali iliyozua wasiwasi katika taaluma ya sheria na kuchochea upya wito wa vyombo vya usalama kuwajibika.
Katika taarifa Rais wa LSK Charles Kanjama amesema aliko Abdi bado hakujulikani licha ya hatua za kisheria na kitaasisi ambazo chama hicho kimeanzisha.
“Chama kina wasiwasi mkubwa kutokana na kutofahamika kwa aliko Wakili Abshir Ahmedsadak Abdi,” Kanjama amesema.
Amesema LSK itatumia njia zote zinazopatikana za kisheria, kitaasisi na hatua nyingine halali hadi wakili huyo atakapopatikana salama na kuunganishwa tena na familia yake pamoja na wenzake, huku waliohusika na kutoweka kwake wakichukuliwa hatua.
LSK imesema iko tayari kwa uamuzi wa Mahakama Kuu ya Milimani Jumanne Tarehe 10 Novemba, kuhusu ombi la kumtafuta na kumwasilisha wakili huyo mahakamani.
Aidha imewataka mawakili kuhudhuria kwa wingi vikao vya mahakama Jumanne kabla ya kuandamana hadi makao makuu ya polisi, kushinikiza hatua zaidi kuhusu uchunguzi wa kutoweka kwa Abshir.
Kufuatia mashauriano katika kikao cha baraza kilichofanyika Jumamosi, Novemba 7, LSK ilitangaza kuwa maandamano itaendelea kuanzia Jumanne.
Chama hicho pia kimewataka mawakili kukamilisha kesi zinazoendelea kufikia saa sita mchana na kuomba kuahirishwa kwa kesi inapohitajika ili kuwawezesha kushiriki katika vikao vya mahakama na maandamano yatakayofuata.
LSK imeonya kuwa kutoweka kwa Abdi si suala linalomhusu mtu mmoja pekee, bali ni tishio kwa taaluma nzima ya sheria na usimamizi wa haki nchini.
“Usalama wa wakili mmoja ni usalama wa taaluma nzima ya sheria. Shambulio dhidi ya mmoja wetu ni shambulio dhidi yetu sote,” imesema taarifa hiyo.









