Ebola Yatinga Nigeria – Kisa cha Kwanza Chathibitishwa.

0
Waziri wa Kuratibu Afya na Ustawi wa Jamii nchini Nigeria, Muhammad Ali Pate.

Taifa la Nigeria limethibitisha kisa chake cha kwanza cha ugonjwa wa Ebola jijini Abuja, baada ya mwanamke aliyesafiri nchini humo kutoka taifa la Uganda kupatikana na virusi hivyo.

Wizara ya Afya nchini Nigeria imethibitisha kisa hicho Jumanne, Oktoba 20, 2026, baada ya vipimo vya maabara kuthibitisha maambukizi hayo.

Katika taarifa, wizara hiyo imesema mwanamke huyo aliwasili Nigeria kwa ndege kutoka Uganda na kwa sasa ametengwa huku akipokea matibabu.

“Serikali ya Shirikisho la Nigeria imethibitisha kisa kimoja cha ugonjwa wa Ebola katika Eneo la Mji Mkuu wa Shirikisho (FCT), kufuatia uthibitisho wa maabara leo, Oktoba 20, 2026,” imesoma sehemu ya taarifa hiyo.

Wizara hiyo imesema inaratibu juhudi za kudhibiti maambukizi hayo kwa ushirikiano na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa nchini Nigeria (NCDC) na mashirika mengine husika.

Tayari Maafisa wa afya wameanza kuwafuatilia watu 44 waliotambuliwa kuwa na uwezekano wa kuwa karibu na mgonjwa huyo na kuwa katika hatari ya kuambukizwa.

Watu hao ni pamoja na wahudumu wa afya, wagonjwa, walezi na watu ambao huenda waliwasiliana na mwanamke huyo wakati wa safari yake.

Wizara ya afya imesema timu za afya ya umma zinaendelea kuwafuatilia watu hao huku hospitali inayomhudumia mgonjwa huyo ikipokea msaada wa haraka wa kuimarisha hatua za kuzuia na kudhibiti maambukizi.

“Ufuatiliaji wa watu waliokuwa karibu na mgonjwa umeanza, huku watu 44 waliokuwa na mawasiliano ya karibu naye wakitambuliwa kufikia sasa.,” imesema wizara hiyo.

Serikali pia imezitaka hospitali za umma na za kibinafsi kote nchini kuongeza umakini, kutambua haraka wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na Ebola, kuwatenga na kuripoti visa hivyo mara moja kwa mamlaka za afya ya umma.

“Wahudumu wa afya wanapaswa kuwa macho zaidi, kutambua na kuwatenga mara moja wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na maambukizi, kuzingatia kikamilifu hatua za kuzuia maambukizi na kuripoti visa vinavyoshukiwa kwa mamlaka za afya ya umma bila kuchelewa,” imesema taarifa hiyo.

Wizara hiyo imesisitiza umuhimu wa kuimarisha tahadhari na kuwataka wananchi kutokuwa na hofu kwani Awali taifa hilo lilifanikiwa kudhibiti mlipuko wa Ebola mwaka 2014, uliosababisha visa 20 vilivyothibitishwa na vifo nane, kabla ya kuzuia kuenea zaidi kwa maambukizi kupitia kuwatenga wagonjwa na kufuatilia watu waliokuwa na mawasiliano nao.

“Nigeria ilifanikiwa kudhibiti Ebola mwaka 2014, na tuna uzoefu pamoja na mifumo ya afya ya umma inayoweza kutusaidia kukabiliana na kisa hiki,” ilisema wizara hiyo.

Kisa hicho kipya kinaibua maswali kuhusu chanzo cha maambukizi ya mwanamke huyo, hasa ikizingatiwa kuwa Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza kumalizika kwa mlipuko wa Ebola nchini Uganda mnamo Agosti 27.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here