Kenya ilianza kampeni ya ubingwa wa dunia kwa utelezi baada ya kupoteza mechi ya kwanza kwa mabao 3-0 dhidi ya Uchina katika kinyanganyiro cha Kombe la Dunia la wasichana walio chini ya umri wa miaka 17 nchini Morocco, Jumatatu tarehe 19 jioni.
Timu ya Junior Starlets, ambayo inashiriki mashindano hayo ya kimataifa kwa mara ya pili, ilianza mchezo kwa kasi na mashambulizi huku shuti la Brenda Achieng kutoka upande wa kulia likipita karibu na lango katika dakika ya nne.
Hata hivyo, matumaini yao yalizimwa katika dakika ya 11 wakati Xu Yue alipopenya nyuma ya safu ya ulinzi ya Kenya na kufunga bao kwa urahisi dhidi ya kipa Mishel Okoyo, aliyekuwa akitoka langoni kujaribu kuzuia shambulizi hilo.
Mashambulizi ya Uchina yaliendelea katika kipindi cha pili baada ya kipindi cha kwanza kukamilika kwa bao hilo moja, huku Xu Xiaotang akiwahi kuudhibiti mpira uliokuwa umerudi uwanjani baada ya kugonga mwamba wa lango na kufunga bao la pili katika dakika ya 50.
Mshambuliaji huyo alikamilisha mabao yake mawili dakika tatu baadaye, akifunga kwa kichwa kwenye lango lililokuwa wazi baada ya kupokea krosi kutoka upande wa kushoto iliyopigwa na Fang Zhenzhu.
Junior Starlets chini ya ukufunzi wa Mildred Cheche sasa watalazimika kujipanga upya mapema kabla ya mechi yao inayofuata dhidi ya Marekani katika uwanja wa Mohammed VI siku ya Alhamisi jioni tarehe 22 Oktoba.









