Idara ya Umisheni ya AIC Yazindua Tovuti Mpya Kupanua Uinjilisti.

0
Viongozi wa Kanisa la AIC na Idara ya Umisheni wakati wa uzinduzi wa Tovuti ya Idara ya Umisheni.

Kanisa la Africa Inland Church (AIC) Kenya limezindua tovuti ya Idara ya Umisheni www.aicmdkenya.org kwa lengo la kupanua wigo wa uinjilisti, kuwafikia vijana na kuhamasisha umma kuunga mkono shughuli za umisheni.

Tovuti hiyo ilizinduliwa Jumapili, Oktoba 18, 2026, wakati wa ibada katika Kanisa la AIC Plainsview, eneo la South B, jijini Nairobi.

Naibu Askofu Mkuu wa Kanisa la AIC Kenya, Kasisi Paul Kirui, amesema uzinduzi huo utaimarisha juhudi za kanisa kueneza injili, hususan miongoni mwa vijana ambao huenda hawajafikiwa vya kutosha na huduma za kawaida za kanisa.

“Uzinduzi wetu utaimarisha uenezaji wa injili ya Bwana wetu Yesu Kristo kwa wale ambao hawajafikiwa,” amesema Kirui.

Ameongeza kuwa kanisa hilo linalenga kuwafikia watu wa makundi mbalimbali, huku likitilia mkazo vijana wa kizazi cha sasa.

“Tunalenga watu wa makundi yote, kwanza vijana, ambao tumekuwa tukiwaacha nyuma hasa wale wenye umri wa kati ya miaka 20 na 40,” amesema.

Mkurugenzi wa Idara ya Umisheni ya AIC, Kasisi Peter Macharia, amesema matumizi ya majukwaa ya kidijitali yamekuwa muhimu ili kuhakikisha watu wengi duniani wanafikiwa na injili kupitia teknolojia.

“Kwa kweli, hatua hii imechelewa. Dunia imekuwa ya kidijitali,” amesema Macharia.

Kasisi Macharia amesema tovuti hiyo itasaidia kanisa kupanua wigo wa huduma zake zaidi.

“Wakati uo huo, tunapaswa kufika hadi mwisho wa dunia. Na ili kufanikisha hilo, hatuwezi kufanikiwa bila kuingia katika ulimwengu wa kidijitali,” amesema.

Macharia amesema jukwaa hilo linalenga hasa vijana na watumiaji wengine wa mitandao ya kijamii, kwa kuwawezesha kupata nyenzo za umisheni na kushiriki katika shughuli za uinjilisti.

Mbali na kuwafikia watu wengi, tovuti hiyo inatarajiwa kusaidia shughuli za uinjilisti, malezi ya kiroho na uanzishaji wa makanisa kwa kutoa nyenzo ambazo watumiaji wanaweza kupata na kuchapisha kwa ajili ya mafunzo.

Macharia amesema nyenzo hizo zitawawezesha waumini kujifunza namna bora ya kueneza injili, kuwalea waumini kiroho na kuanzisha makanisa.

Kwa upande wake, Afisa Msimamizi wa Kitaifa wa Kanisa la AIC Kenya, Kasisi Daktari Simeon Adera, amesema tovuti hiyo itatoa taarifa kuhusu maono, malengo, na programu za Idara ya Umisheni, pamoja na shughuli za wamishonari na jamii wanazohudumia.

“Kupitia tovuti hii, tutaunga mkono kazi ya umisheni kwa kuweka wazi maono yake, malengo, misingi ya maadili na programu zake,” amesema Adera.

“Taarifa kuhusu wamishonari wetu na maeneo wanakohudumu, pamoja na mahitaji yao, zitapatikana ili kuwawezesha wananchi kuwaombea, kuwapa msaada wa kifedha na kuwaunga mkono kwa njia nyingine,” amesema.

Kupitia uzinduzi huo, AIC Kenya inalenga kuunganisha mawasiliano ya kidijitali na juhudi zake za uinjilisti ili kuwafikia watu walio nje ya mazingira ya kawaida ya kanisa na kuhamasisha msaada zaidi kwa jamii ambazo bado hazijafikiwa na injili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here