Katibu katika Wizara ya Mambo ya Nje, Korir Sing’Oei, ametetea utaratibu wa kutangaza matokeo ya uchaguzi mubashara, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kujenga imani ya wananchi kwa mfumo wa uchaguzi nchini Kenya na kuimarisha imani ya kimataifa kuhusu uchaguzi wa Kenya.
Sing’Oei amesema usambazaji wa matokeo kwa wakati halisi umechangia kuimarisha uwazi katika uchaguzi na unapaswa kuboreshwa badala ya kuondolewa kutokana na changamoto za kiteknolojia.
“Kwa mtazamo wangu, katika suala la uwazi na imani ya kimataifa kuhusu uchaguzi wa Kenya, uwezo wetu wa kusambaza matokeo kwa wakati halisi umekuwa mojawapo ya mambo yaliyochangia,” amesema Sing’Oei.
Amesema ingawa kumekuwa na wasiwasi kuhusu hitilafu za kiteknolojia na hatari za usalama wa mifumo ya kielektroniki, changamoto hizo zinapaswa kutatuliwa bila kuachana na utaratibu wa kutangaza matokeo mubashara.
“Tungependa kuona utaratibu huo ukiimarishwa badala ya kuondolewa kwa sababu ya changamoto zinazohusiana na teknolojia,” amesema.
Sing’Oei ameongeza kuwa hitilafu za teknolojia zinaweza kuzua hofu na wasiwasi miongoni mwa wapiga kura, hasa pale maswali yanapozuka kuhusu uadilifu na uaminifu wa matokeo ya uchaguzi.
“Kunaweza kuwa na hitilafu za kiteknolojia ambazo zimebainika na zinazoweza kuzua hofu na wasiwasi. Pia kunaweza kuwa na changamoto za usalama wa mifumo ya kielektroniki, lakini masuala hayo yanapaswa kushughulikiwa na kutatuliwa,” ameongeza.
Amesisitiza kuwa changamoto hizo hazipaswi kutumiwa kama sababu ya kuondoa utaratibu wa kutangaza matokeo mubashara.
“Masuala haya hayapaswi kuwa sababu ya kuondoa utaratibu wa kutangaza matokeo mubashara. Mimi ninaunga mkono utaratibu huo,” ameongeza. `
Kauli ya Sing’Oei inajiri wakati wabunge wanatarajiwa kujadili mapendekezo ya kuondoa sharti la kisheria linaloitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuweka utaratibu wa kutangaza mubashara matokeo yanayotangazwa katika vituo vya kupigia kura.
Mapendekezo hayo yamo katika Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi wa mwaka 2024, ambao umeidhinishwa na Seneti na sasa uko katika Bunge la Kitaifa kwa ajili ya kujadiliwa na kuafikiwa.
Mswada huo unapendekeza kufuta na kuweka upya Kifungu cha 39 cha Sheria ya Uchaguzi, kinachohusu usambazaji, uthibitishaji na utangazaji wa matokeo ya uchaguzi.
Mabadiliko hayo yangeondoa sharti linaloitaka IEBC kuweka utaratibu wa kutangaza mubashara matokeo yanayotangazwa katika vituo vya kupigia kura.
Mjadala huo unafuatia uamuzi wa Mahakama Kuu wa Aprili 6, 2018, uliotangaza kuwa kinyume cha Katiba marekebisho ya sheria yaliyotaka matokeo yanayotangazwa mubashara kuchukuliwa kama taarifa kwa umma pekee, badala ya kuwa msingi wa kutangaza mshindi.
Uamuzi huo, ambao baadaye uliungwa mkono na Mahakama ya Rufaa, ulionyesha kuwa kifungu hicho kilidhoofisha uwazi na uwajibikaji katika mchakato wa uchaguzi.
Sasa, badala ya kurekebisha kifungu hicho kwa kuzingatia uamuzi wa mahakama, mapendekezo yaliyoko mbele ya Bunge yanataka kuondoa sharti la kutangaza matokeo mubashara katika sheria.
Mswada huo ukipitishwa, IEBC haitakuwa tena na sharti hilo mahususi la kisheria la kuweka utaratibu wa kutangaza matokeo ya vituoni vya kupigia kura mubashara.
Hata hivyo, mjadala unaendelea kuhusu namna ya kuhakikisha uwazi na uaminifu wa mchakato wa uchaguzi huku changamoto za kiteknolojia na usalama zikiangaziwa.









