Onyo Latolewa Kwa Viongozi Dhidi ya Uchochezi Kulekea Uchaguzi Mkuu 2027.

0
Mwenyekiti wa NCIC Askofu Kepha Nyamweya Omae

Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) imewaonya viongozi wa kisiasa dhidi ya kutumia mikutano ya hadhara kueneza uchochezi, vitisho na matamshi ya chuki kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Katika taarifa Mwenyekiti wa tume hiyo, Askofu Kepha Nyamweya Omae, amesema kuongezeka kwa joto la kisiasa hakupaswi kuwa sababu ya viongozi kugeuza mikutano ya hadhara kuwa majukwaa ya makabiliano na vurugu.

Omae amesisitiza kuwa ingawa Katiba inalinda uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani, haki hizo hazipaswi kutumiwa kuhalalisha uchochezi, matamshi ya chuki au kuvuruga shughuli za wengine.

“Hata pale ambapo kuna kutokubaliana, mjadala unapaswa kuzingatia hoja badala ya kushambulia watu binafsi,” amesema Omae.

NCIC imewataka viongozi wa kisiasa kudhibiti wafuasi wao na kuhakikisha mikutano yao inaendeshwa kwa utulivu.

Omae amesema viongozi wanapaswa kuwajibika kwa mienendo ya wafuasi wao, akiwataka kukomesha vitendo vinavyoweza kuchochea vurugu na kuhatarisha usalama wa wananchi.

Kadhalika Tume hiyo imesema inaendelea kufuatilia mikutano ya kisiasa pamoja na majukwaa ya kidijitali ili kubaini na kukabiliana na matamshi yanayoweza kuchochea chuki na migawanyiko miongoni mwa Wakenya.

NCIC pia imezitaka vyama vya kisiasa kuhakikisha wanachama na wafuasi wao wanafuata kanuni za maadili ya uchaguzi vijana wakionywa dhidi ya kuruhusu kutumiwa na wanasiasa kuendeleza vurugu au kuvuruga mikutano ya hadhara.

Aidha, vyombo vya usalama vimetakiwa kutekeleza majukumu yao bila upendeleo, huku vyombo vya habari vikihimizwa kuepuka kusambaza ujumbe wa uchochezi na taarifa ambazo hazijathibitishwa.

NCIC imeonya kuwa itachukua hatua za kisheria dhidi ya watu wanaohusika na uchochezi, matamshi ya chuki na ufadhili wa vurugu kwa mujibu wa Sheria ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa ya mwaka 2008.

Tume hiyo imesema juhudi zake ni sehemu ya kampeni ya “Uchaguzi Bila Noma,” inayolenga kuhimiza amani, uvumilivu na mshikamano wa kitaifa kabla, wakati na baada ya uchaguzi wa 2027.

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here