ACA Yaongeza Vita Dhidi ya Bidhaa Bandia humu Nchini.

0
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Kupambana na Bidhaa Bandia ACA, Nelson Ribuithi Gaichuhie na Mkurugenzi Mtendaji wa ACA Robi M. King’a,

Mamlaka ya Kupambana na Bidhaa Bandia nchini (ACA) imeongeza operesheni kote nchini kulenga bidhaa bandia na haramu, zikiwemo pombe, bidhaa za afya na pembejeo za kilimo.

Mwenyekiti wa Bodi ya ACA, Nelson Ribuithi Gaichuhie, amesema biashara ya bidhaa bandia inahatarisha afya ya umma, usalama wa watumiaji na biashara halali.

“Biashara ya bidhaa bandia na haramu ina gharama kubwa ambayo haiwezi kupimwa kwa fedha pekee.” Amesema Gaichuhie.

Kwa mujibu wa Gaichuhie, Operesheni za pamoja zilizofanyika kati ya Agosti 20 na Septemba 3, 2026, zilisababisha kukamatwa kwa washukiwa 36, huku zaidi ya chupa 5,555 za pombe zinazoshukiwa kuwa bandia na takriban lita 39,580 za pombe haramu zikikamatwa katika maeneo mbalimbali jijini Nairobi.

Operesheni nyingine mwezi Septemba zilisababisha kukamatwa kwa bidhaa za pombe zinazoshukiwa kuwa bandia zenye thamani ya shilingi milioni 2.1 mjini Makindu.

Bidhaa nyingine zilizokamatwa Nairobi, Nyeri na maeneo mengine zilifikisha thamani ya bidhaa zilizokamatwa mwezi huo hadi takriban shilingi milioni 3.74.

Katika eneo la Matungu, kaunti ya Kakamega, maafisa wa ACA pia walikamata mbolea inayoshukiwa kufungashwa upya kinyume cha sheria, malori mawili na vifaa vya kufungashia bidhaa.

Nelson ameeleza kuwa kwa mujibu wa uchunguzi wa awali mbolea hiyo huenda ilielekezwa kinyume cha utaratibu kutoka kwa mpango wa serikali wa kutoa ruzuku ya mbolea, kisha kufungashwa katika mifuko yenye chapa bandia ili kuuzwa kwa bei ya kawaida ya soko.

Mkurugenzi Mtendaji wa ACA, Robi M. King’a, naye amesema sehemu kubwa ya bidhaa bandia zinazoingia katika soko la Kenya hutoka nje ya nchi.

“Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 70 ya bidhaa zote bandia hutoka nje ya Kenya.” King’a amesema.

King’a amesema mamlaka hiyo inashirikiana na polisi, Mamlaka ya Ushuru nchini (KRA), Shirika la Kukadiria Viwango vya bidhaa humu nchini (KEBS), Wizara ya Afya na mashirika mengine kuimarisha ukaguzi na kuzuia bidhaa haramu kuingia sokoni, ikiwemo kupitia maeneo ya mipaka yenye mianya ya kiusalama.

Amesema ACA inaandaa mfumo jumuishi wa usimamizi wa kupambana na bidhaa bandia, utakaosaidia kuhakiki bidhaa zinazoagizwa kutoka nje kabla ya kuingia nchini.

Mamlaka hiyo pia inapanga kuzindua mpango utakaowawezesha wamiliki wa chapa za biashara kusajili taarifa zao, ili kurahisisha uhakiki wa chapa halisi na kusaidia kupambana na bidhaa bandia mwezi Novemba 2026

Wakati uo huo King’a Amewaonya wafanyabiashara dhidi ya kuendeleza biashara ya bidhaa bandia wakati wa msimu wa sherehe.

“Hatutawaruhusu kuzalisha na kusambaza bidhaa bandia.” Ameongeza.

ACA imewataka wananchi kununua bidhaa katika maduka yaliyoidhinishwa na yanayoaminika na kuthibitisha alama za viwango kupitia njia rasmi.

Wakulima pia wameshauriwa kupata mbolea ya ruzuku kutoka kwa wauzaji walioidhinishwa pekee, huku wananchi wakihimizwa kuripoti bidhaa zinazoshukiwa kuwa bandia kwa ACA au katika ofisi zake humu nchini.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here