Waziri wa Elimu Julius Migos Ogamba ameonya dhidi ya udanganyifu katika mitihani ya kitaifa, akisema serikali itachukua hatua za kisheria dhidi ya yeyote atakayepatikana akijihusisha na ukiukaji wa taratibu za mitihani huku zaidi ya wanafunzi milioni 2.4 wa Gredi ya Sita na Gredi ya Tisa wakianza mitihani yao nchini.
Akizungumza kaunti ya Makueni Jumatatu, Oktoba 26, wakati wa usambazaji wa karatasi za kwanza za mitihani, Ogamba amewaonya wazazi, watahiniwa na umma dhidi ya watu wanaodai kuwa na uwezo wa kupata karatasi za mitihani kabla ya wakati na kuziuza kwa nia ya kuwasaidia watahiniwa kutekeleza udanganyifu.
“Ninawaonya wazazi, watahiniwa na wanajamii dhidi ya watu wanaodai kuwa na uwezo wa kupata karatasi za mitihani kabla ya wakati na kudai pesa kwa ahadi ya kuwapa karatasi hizo. Madai hayo ni ya ulaghai,” amesema Ogamba.
Ogamba amewataka walio na taarifa kuhusu watu wanaouza mitihani hiyo bandia kuripoti kwa mamlaka husika ili hatua zichukuliwe.
“Ninawasihi wote walio na taarifa kuhusu shughuli hizi kuripoti mara moja kwa mamlaka husika,” ameongeza.
Ogamba pia amesisitiza kuwa serikali haitavumilia udanganyifu wa aina yoyote wakati wa mitihani ya mwaka huu, akiwataka wasimamizi wa vituo, wasimamizi wa mitihani na maafisa wengine kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na weledi wa hali ya juu.
“Mtu yeyote atakayepatikana akijihusisha na ukiukaji wa taratibu za mitihani atachukuliwa hatua zinazofaa za kisheria,” amesema.
Ameongeza kuwa serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha tathmini hizo zinafanyika katika mazingira salama, ya haki na yanayoaminika, huku wanafunzi wenye ulemavu na wanaohitaji usaidizi maalum wakipewa mazingira yanayowawezesha kufanya mitihani yao.









