Serikali imetangaza kuwapandisha vyeo walimu elfu hamsini ndani ya mwaka wa kifedha 2026/27, hatua iliyotajwa kuwa zoezi kubwa zaidi la aina hiyo kufanywa ndani ya mwaka mmoja nchini Kenya.
Rais William Ruto amesema Tume ya Huduma za Walimu (TSC) tayari ilikuwa imetangaza nafasi 34,016 za kupandishwa vyeo, lakini akaagiza idadi hiyo iongezwe hadi 50,000.
“Serikali itatoa ufadhili wa ziada ili kuhakikisha hili linawezekana,” alisema rais William Ruto.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya walimu duniani jijini Nairobi Jumatatu tarehe 5, Oktoba, rais Ruto amesema serikali imeongeza mara mbili bajeti ya upandishaji vyeo walimu kutoka shilingi bilioni moja hadi shilingi bilioni mbili.
Wakati huo huo, rais Ruto amesema mapitio ya miongozo mipya ya maendeleo ya taaluma ya walimu yamekamilishwa na TSC pamoja na vyama vya walimu, na sasa yanasubiri kuidhinishwa na Tume ya Mishahara (SRC).
Rais zaidi amebainisha kuwa uwekezaji katika elimu umeongezeka kutoka shilingi bilioni 526 katika mwaka wa kifedha wa 2021/22 hadi shilingi bilioni 702 mwaka 2025/26, na sasa umefikia zaidi ya shilingi bilioni 784.5, hivyo kuifanya elimu kuwa sekta inayopokea mgao mkubwa zaidi katika bajeti ya kitaifa.
Alisema uwekezaji huo ulioongezeka unalenga kuimarisha mfumo wa elimu na kuboresha ustawi wa walimu, maendeleo yao kitaaluma pamoja na mazingira ya kazi.
Amebainisha kuwa serikali imeajiri walimu 100,000 katika kipindi cha miaka minne iliyopita, huku wengine 20,000 wakitarajiwa kuajiriwa kufikia Desemba 2026.
Aidha, kiongozi wa taifa amesema serikali imetenga fedha kuwaajiri walimu 20,000 ambao wamehudumu kwa muda wa miaka miwili kama wanagenzi, kuanzia Januari 2027.
Kuhusu suala la afya serikali imetaja kuimarisha bima ya matibabu ya walimu chini ya Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), na kuongeza kiwango cha huduma za kulazwa hospitalini kutoka asilimia 7 hadi asilimia 14.
Kuhusu umiliki wa nyumba, kiongozi wa taifa alisema asilimia 20 ya nyumba za bei nafuu zimetengewa walimu chini ya makubaliano yaliyotiwa saini kati ya bodi ya nyumba za bei nafuu, na vyama vya walimu vya KNUT na KUPPET.









