Waziri wa Elimu Julius Ogamba amewaagiza wahadhiri wa vyuo vikuu vya umma walio kwenye mgomo kurejea kazini mara moja
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani Jumatatu Oktoba 5 2026 Ogamba amesema serikali imetekeleza sehemu kubwa ya matakwa ya wahadhiri
Ogamba ameongeza kuwa serikali tayari imelipa malimbikizi ya mishahara na marupurupu yaliyotokana na mikataba ya makubaliano ya Pamoja CBA ya mwaka 2017–2021 na 2021–2025.
“Serikali imejitolea kulinda maslahi ya wahadhiri wote na imeonyesha dhamira hiyo kupitia hatua. Kufikia sasa, malimbikizo yote chini ya CBA za 2017–2021 na 2021–2025 yamelipwa,” amesema Ogamba.
Aidha amesema serikali iko tayari kuendelea na mazungumzo kuhusu mikataba ijayo, ikiwemo CBA ya 2025–2029.
“Tumejitolea kuhakikisha mazungumzo ya mikataba yote ijayo yanafanyika kwa wakati na kukamilishwa, ikiwemo CBA ya 2025–2029,” ameongeza.
Ogamba ameutaka Muungano wa wahadhiri wa vyuo vikuu nchini UASU na wahadhiri binafsi kutii maagizo ya mahakama na kurejea kazini, akisema maslahi ya wanafunzi hayafai kuathiriwa na mzozo huo.
“Natoa wito kwa UASU na wahadhiri binafsi kutii maagizo ya mahakama na kurejea kazini. Tusikatishe masomo ya wanafunzi wetu kuhusu masuala ambayo serikali imeonyesha iko tayari na ina nia ya kuyatatua kupitia mazungumzo,” ameongeza.
Wahadhiri wa vyuo vikuu vya umma walianza mgomo wa kitaifa Ijumaa, Oktoba 2, wakilalamikia kutotekelezwa kwa Mkataba wa Makubaliano CBA ya Mwaka 2025–2029.
Katibu Mkuu wa UASU, Constantine Wasonga, alisema mgomo huo unatokana na kushindwa kwa serikali kutekeleza mkataba huo pamoja na Makubaliano ya Kurejea Kazini yaliyotiwa saini Novemba 5, 2025.
UASU pia inadai serikali imeshindwa kutoa pendekezo la kifedha kuhusu CBA ya 2025–2029, licha ya mazungumzo kuendelea tangu mwaka jana.









