SHA Yaongeza Siku 14 Kwa Hospitali Kukamilisha Mikataba Mipya.

0
Afisa Mkuu Mtendaji wa SHA, Dkt. Mercy Mwangangi
Afisa Mkuu Mtendaji wa SHA, Dkt. Mercy Mwangangi

Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA, imeongeza kwa siku 14 muda wa vituo vya afya kukamilisha mchakato wa mikataba mipya, na kusogeza tarehe ya mwisho kutoka Septemba 30 hadi Oktoba 14, 2026.

Hatua hiyo inalenga kuzipa hospitali na vituo vya afya muda zaidi kukamilisha mchakato wa kuingia katika mikataba ya utoaji huduma kwa kipindi cha 2026–2029.

Afisa Mkuu Mtendaji wa SHA, Dkt. Mercy Mwangangi, amesema vituo vya afya vitaendelea kutoa huduma kwa wanufaika wa SHA chini ya mikataba yao ya sasa katika kipindi hicho cha siku 14.

“Katika kipindi cha nyongeza, vituo vya afya vitaendelea kufanya kazi chini ya mikataba yao iliyopo,” amesema Mwangangi.

SHA imesema watoa huduma watapewa nyongeza ya mikataba yao kupitia mfumo wa kielektroniki wa SHA na wanatakiwa kuthibitisha, kukubali, kutia saini na kurejesha makubaliano hayo ndani ya siku tatu ili kuhakikisha huduma zinaendelea bila kukatizwa.

Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa vituo ambavyo havitakubali nyongeza hiyo vinapaswa kuwasiliana na wasimamizi wa SHA katika kaunti zao ili kupanga uhamishaji wa wagonjwa wanaoendelea na matibabu kwenda katika vituo vilivyo na mikataba halali.

“Baada ya siku hizo 14, mikataba iliyopo itakoma na hakutakuwa na nyongeza nyingine,” amesema Mwangangi.

Kwa mujibu wa SHA, watoa huduma wanaotaka kupata mikataba mipya ya miaka mitatu wanapaswa kukamilisha mchakato kupitia mfumo wa kidijitali wa SHA na kutimiza masharti yaliyowekwa, ikiwemo kuwa na mifumo ya kidijitali iliyothibitishwa inayounganishwa moja kwa moja na Mamlaka ya Afya ya Kidijitali.

Mikataba hiyo inahusisha huduma zinazolipiwa kupitia Hazina ya Bima ya Afya ya Jamii, SHIF, pamoja na Hazina ya Huduma ya Afya ya Msingi, PHCF.

SHA pia imesema watoa huduma 10,006 tayari wameonyesha nia ya kuingia katika mikataba mipya na wako katika hatua mbalimbali za mchakato huo.

SHA imeonya kuwa baada ya Oktoba 14, vituo ambavyo havitakuwa vimekamilisha na kutia saini mikataba mipya havitaruhusiwa kuendelea kutoa huduma kwa wanufaika wa SHA.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here