Rais William Ruto ametuma risala za rambirambi kufuatia kifo cha mfanyabiashara maarufu wa Zimbabwe, Wicknell Chivayo na mkewe Lucy Muteke, waliokufa katika ajali ya helikopta nchini Zimbabwe.
“Nimehuzunishwa sana na kifo cha ghafla cha rafiki yangu, Wicknell Chivayo, pamoja na mkewe Lucy Muteke na watu wengine waliopoteza maisha katika ajali hiyo ya helikopta nchini Zimbabwe.” Rais Ruto amesema.
Rais Ruto amesema Chivayo alikuwa rafiki yake wa karibu ambaye atamkumbuka kwa imani yake kuhusu uwezo wa bara la Afrika.
“Wicknell alikuwa rafiki wa karibu ambaye uchangamfu wake uliwagusa watu wengi. Nitakumbuka imani yake kubwa katika uwezo wa bara letu,” ameongeza.
Rais pia ametuma risala za rambirambi kwa familia za wote waliofariki, Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa na wananchi wa Zimbabwe.
Chivayo na mkewe Lucy Muteke walikuwa miongoni mwa watu sita waliofariki baada ya helikopta waliyokuwa wakisafiria kuanguka katika eneo la Marondera, takriban kilomita 70 mashariki mwa mji mkuu Harare, Jumatano jioni tarehe 30 Septemba.
Kwa mujibu wa taarifa, helikopta hiyo ilikuwa imeondoka Gandami, eneo la Chikomba, kabla ya kuanguka katika shamba la Kudenga, takriban dakika 40 baada ya kupaa.
Mamlaka za Zimbabwe zimesema hakukuwa na manusura, huku uchunguzi ukianzishwa kubaini chanzo cha ajali hiyo.
Chivayo alikuwa ameonekana mara kadhaa pamoja na Rais Ruto nchini Kenya, ikiwa ni pamoja na katika mikutano ya Ikulu na ziara katika makazi ya Rais huko Kilgoris, Narok.









