Msomi maarufu wa sheria nchini Profesa Patrick Loch Otieno Lumumba, ametoa wito wa kufanyika kwa marekebisho katika mfumo wa serikali za ugatuzi nchini, akipendekeza idadi ya kaunti ipunguzwe kutoka 47 hadi 14 ili kupunguza gharama ya kuendesha serikali.
Lumumba amesema muundo wa sasa wa serikali nchini ni wa gharama kubwa, huku rasilimali nyingi zikitumika katika kuendesha taasisi na miundo mbalimbali ya utawala.
Amesema Kenya inahitaji kutafakari upya namna serikali inavyoendeshwa ili kupunguza matumizi na kuhakikisha fedha za umma zinaelekezwa zaidi katika maendeleo na utoaji wa huduma.
“Tuna mfumo wa serikali ambao ni wa gharama kubwa kuendesha. Uamuzi tunaopaswa kufanya ni jinsi ya kupanga upya na kufikiria upya mfumo wa utawala. Kaunti hizi 47 tulizonazo zinapaswa kupunguzwa hadi 14,” amesema Profesa PLO Lumumba.
Lumumba pia amehoji gharama ya kuendesha serikali za kaunti, akisema mishahara ya viongozi pamoja na miundo ya utawala ni miongoni mwa maeneo yanayopaswa kuangaziwa sana katika juhudi za kupunguza matumizi ya fedha za umma.
Kwa mujibu wa muundo wa malipo wa Tume ya Mishahara na Marupurupu, SRC, Gavana hupokea mshahara wa msingi pamoja na marupurupu unaofikia takriban shilingi 957,000 kwa mwezi.
Hii ina maana kwamba kila mwezi serikali hugharamika takriban shilingi milioni 44.98 katika mishahara na marupurupu ya magavana wote 47.
Kupunguzwa kwa idadi ya kaunti kunaweza kupunguza baadhi ya gharama za uongozi na uendeshaji wa serikali za kaunti, kwa kuwa kutakuwa na miundo michache ya kiutawala na nafasi chache za uongozi.
Pendekezo la kupunguza idadi ya kaunti litahitaji mabadiliko makubwa ya kikatiba na kisheria.
Pia huenda likazua mjadala kuhusu uwakilishi wa wananchi, upatikanaji wa huduma, mgawanyo wa rasilimali na muundo wa uongozi katika maeneo mbalimbali nchini.









