Wazee wa vijiji nchini wataanza kupokea malipo ya kila mwezi ya shilingi 3,000, ikiwa ni mara ya kwanza kwa serikali kuwaweka rasmi wasimamizi hao wa ngazi ya chini katika mpango huo ulioratibiwa kama sehemu ya juhudi za kuimarisha utawala wa maeneo ya msingi na utoaji wa huduma.
Rais William Ruto alitangaza mpango huo Jumanne tarehe 4 Agosti 2026 alipokutana na wazee hao kutoka sehemu mbalimbali za nchi uliofanyika ikuluni, Nairobi akisema kuwa serikali imejitolea kuboresha ustawi wao na kuimarisha nafasi yao katika mfumo wa utawala wa serikali ya kitaifa.
“Kuanzia leo, kila mzee wa kijiji atalipwa posho ya kila mwezi ya Shilingi 3,000,” alisema rais Ruto.
Rais pia alielekeza kwamba wazee wote wa vijiji pamoja na familia zao za karibu waandikishwe katika mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), huku serikali ikiahidi kugharamia michango yote hitajika.
“Kila mzee wa kijiji na familia yake wataandikishwa katika SHA, na serikali italipia michango inayohitajika,” alisema.
Aidha, kiongozi wa taifa vilevile alitangaza kuwa wazee wa vijiji watapatiwa mafunzo ya matumizi ya teknolojia ya kidijitali pamoja na kupewa vifaa vya mawasiliano ya kidijitali ili kuboresha uratibu wao na machifu, manaibu wa machifu pamoja na taasisi nyingine za serikali.
Pia aliiagiza wizara ya mambo ya ndani kuharakisha mchakato wa kutunga sheria ambayo ingeitambua rasmi nafasi ya mzee wa kijiji kisheria, na kuwapa mamlaka ya wazi ndani ya mfumo wa utawala wa nchi.
Tangazo hilo liliendeleza mfumo wa sera uliotayarishwa na wizara ya mambo ya ndani wenye lengo la kuwatambua rasmi, kuwasajili na kuwaunganisha wazee wa vijiji katika mfumo wa utawala wa serikali ya kitaifa.
Mfumo huo, ambao ulikuwa ukiandaliwa kwa karibu mwongo mmoja kufuatia mapendekezo ya bunge yaliyotolewa mwaka 2016, unalenga kuweka viwango vya pamoja vya namna ya kuwaajiri na kuwapa majukumu wazee wa vijiji huku ukitambua mchango wao wa muda mrefu katika utawala wa umma.
Mpango huu unatarajiwa kuwanufaisha takriban wazee wa vijiji 110,000 kote nchini, ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakihudumu kwa kujitolea kama kiungo cha kwanza katika kutatua migogoro ya jamii, kuhamasisha wananchi kushiriki katika mipango ya serikali, kusaidia vyombo vya usalama katika ukusanyaji wa taarifa na kuwasaidia machifu katika shughuli za utawala wa maeneo yao bila kulipwa rasmi.
Bunge liliidhinisha fedha za kutekeleza mpango huu katika mwaka wa kifedha wa 2026/27 baada ya wabunge kuunga mkono pendekezo la kutenga fedha zilizohitajika za kuuwezesha.
Katika hafla hiyo waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Kipchumba Murkomen, alisema kuwa serikali pia ilikuwa ikiendelea kuimarisha maafisa wa Utawala wa Serikali ya Kitaifa (NGAO) kwa kuongeza fedha za shughuli za machifu na manaibu wa machifu.
“Katika robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha, tumeongeza mgao wa Mamlaka ya Kutumia Fedha (AIE) kwa manaibu wa machifu kutoka shilingi 15,000 hadi shilingi 30,000, na kwa machifu kutoka Shilingi 30,000 hadi shilingi 50,000,” alisema Murkomen.
Aliongeza kuwa serikali ilikuwa imepeleka maafisa 6,000 wa kitengo cha Polisi cha Utawala wa Serikali ya Kitaifa (NGAPU) katika kaunti ndogo 16 ili kuimarisha usalama wa machifu na manaibu wa machifu, huku kukiwa na mpango wa kuongeza idadi hiyo baada ya kundi jingine la maafisa kuhitimu mafunzo.
Murkomen aliwahimiza wazee wa vijiji kutekeleza majukumu yao kwa haki bila upendeleo, kuzingatia maadili ya katiba na kuendelea kuimarisha amani, mshikamano wa kitaifa na utoaji bora wa huduma katika ngazi ya jamii.
Kulingana na serikali mageuzi hayo yalilenga kuunda mfumo imara zaidi na wenye mwitikio wa haraka wa utawala wa ngazi ya chini kwa kuwatambua rasmi wazee wa vijiji, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitekeleza majukumu yao kwa kujitolea licha ya nafasi yao muhimu katika uongozi wa jamii, utatuzi wa migogoro na utekelezaji wa programu za serikali.









