Zaidi ya wanasiasa 15 wanaodaiwa kuhusishwa na matamshi ya chuki na uchochezi huenda wakazuiwa kuwania nyadhifa mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.
Hatua hiyo inafuatia kuundwa kwa kamati ya pamoja inayojumuisha Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC), Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa pamoja na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).
Kamati hiyo itaratibu juhudi za taasisi hizo katika kukabiliana na matamshi ya chuki na uchochezi kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
Mwenyekiti wa NCIC, Dkt. Askofu Kepha Omae, amesema jopo hilo litasimamia uchunguzi, kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa viongozi watakaobainika kukiuka sheria kwa kutoa matamshi ya chuki au uchochezi.
“Tunawakumbusha viongozi wote na wananchi kwamba ingawa Katiba inahakikisha haki ya uhuru wa kujieleza, haki hiyo si ya bila mipaka. Haihusishi propaganda, uchochezi na vurugu, matamshi ya chuki wala uhamasishaji wa chuki.” Askofu Kepha Omae amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa IEBC Erastus Edung Ethekon amesema tume hiyo itatangaza rasmi ratiba ya uchaguzi, ikiwemo kipindi cha kampeni, baadaye mwezi huu.
Aidha ameonya kuwa uchaguzi wa huru na wa haki hauwezi kufanyika katika mazingira yaliyojaa migawanyiko, vurugu na matamshi ya uchochezi.
“Ningependa kuweka wazi kwamba IEBC haiwezi kuendesha uchaguzi katika mazingira yaliyojaa uchochezi, migawanyiko, vurugu, machafuko na hali ya ukosefu wa utawala wa sheria,” amesema Ethekon.
Naye Mkurugenzi wa DCI Mohamed Amin amewaonya wanasiasa wanaotumia mikutano ya kisiasa na mitandao ya kijamii kutoa matamshi ya uchochezi, akisema idara hiyo itawachukulia hatua kali za kisheria wote watakaopatikana wamekiuka sheria bila kujali nyadhifa zao.
Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Kisiasa John Cox Lorionokou pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Jukwaa la Vyama vya Kisiasa, Evans Misati, walisema viongozi watakaopatikana wamekiuka sheria za uchaguzi na maadili ya viongozi kwa kutoa matamshi ya chuki au uchochezi huenda wasiruhusiwe kushiriki uchaguzi wa mwaka 2027.
Viongozi hao wamesisitiza kuwa taasisi zote zinazohusika zitaimarisha ushirikiano katika kutekeleza sheria kwa usawa, kwa lengo la kuhakikisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 unafanyika katika mazingira ya amani, uwazi na kuheshimu utawala wa sheria.









