Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya umeanza rasmi mchakato wa kujijenga upya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027, kwa kuvikaribisha vyama vipya vya kisiasa na kuanzisha mazungumzo na makundi mengine ya upinzani yanayoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna.
Katika mkutano wa Baraza la Azimio ulioongozwa kwa njia ya mtandao na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, viongozi wa muungano huo walikubaliana kufanya mabadiliko makubwa yatakayojumuisha kubadilisha jina la Azimio na kupanua wigo wake ili kuwaunganisha wadau wote wa upinzani kabla ya kumteua mgombea mmoja wa urais atakayechuana na Rais William Ruto mwaka 2027.
Kama sehemu ya mageuzi hayo, vinara wa kisiasa akiwemo Fred Matiang’i wa Jubilee, Peter Munya wa PNU na aliyekuwa Seneta wa Embu Lenny Kivuti wamejumuishwa katika Baraza la Muungano huo.
Aidha, chama cha DP kinachoongozwa na aliyekuwa Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi, pamoja na chama cha UMP chake aliyekuwa Gavana wa Meru Kawira Mwangaza, vimekubaliwa rasmi kujiunga na Azimio.
Muungano huo pia umekikaribisha tena chama cha DAP-K kinachoongozwa na Eugene Wamalwa, baada ya kusitisha mchakato wake wa kujiondoa Azimio.
Katibu Mkuu wa Azimio, Caroli Omondi, amesema viongozi wamekubaliana kuanzisha mazungumzo rasmi na chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) kinachoongozwa na Rigathi Gachagua pamoja na vuguvugu la Linda Mwananchi linalohusishwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, kwa lengo la kuunda muungano mpana zaidi wa upinzani.
Caroli ameongeza kuwa Azimio pia inaendelea na mazungumzo na aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga, ambaye ni Kinara wa chama cha United Green Movement (UGM).
Ameongeza kuwa vuguvugu la Linda Mwananchi linatarajiwa kujiunga rasmi na muungano huo baada ya kukamilisha usajili wake kama chama cha kisiasa.
Kwa mujibu wa Omondi, Linda Mwananchi ndilo litakalojaza nafasi iliyoachwa na ODM ndani ya Azimio kufuatia mabadiliko ya kisiasa yaliyokikumba chama hicho.
“Tumeamua kupanga upya muungano na kuanza mchakato wa kubadilisha sura na jina la Azimio ili liwe jukwaa linalowakutanisha washirika wote wa upinzani,” amesema Caroli.
Pia amekanusha madai kuwa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta ndiye anayesimamia mikakati ya kisiasa ya upinzani, akisema nafasi yake ni kutekeleza wajibu wake kama mwenyekiti wa muungano.
Mabadiliko hayo yanalenga kuufanya muungano huo uwe na mvuto kwa wafuasi wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, vijana wa kizazi cha Gen Z pamoja na makundi mapya ya kisiasa.









