Aliyekuwa Waziri wa Fedha Njuguna Ndung’u amemshutumu Rais William Ruto kwa Kudhoofisha Taasisi za Serikali, kwa kuweka mamlaka mengi katika Ofisi ya Rais.
Akizungumza katika mkutano wa ushirikiano wa maendeleo nchini Sweden, Ndung’u amesema taasisi nyingi za serikali hazifanyi kazi kwa uhuru tena kwa sababu maafisa wa umma wanaogopa kumpinga Rais.
Kwa mujibu wa Ndung’u, kuwekwa kwa mamlaka mengi katika Ofisi ya Rais kumedhoofisha mfumo wa uwajibikaji, utawala bora na uhuru wa taasisi za umma.
“Uwezo wa kufanya mambo sahihi upo, lakini umefunikwa na tatizo la kushindwa kwa taasisi, ambapo kuna mtu anataka kuongoza kila taasisi na kudhoofisha mamlaka ya taasisi hizo.”
“Rais wa sasa anaingilia taasisi zote za serikali, na ndiyo maana kila mtu katika taasisi hizo analazimika kufuata matakwa yake kwa sababu ya hofu.”
Ndung’u pia amedai kuwa alipokuwa Waziri wa Fedha alishinikizwa kuidhinisha mikataba yenye utata, lakini alikataa akisema dhamiri yake haikumruhusu kushiriki katika miamala aliyodhani haikuwa halali swala lililosababisha kupigwa kalamu.
“Nilikataa kutekeleza mikataba yenye utata katika Wizara ya Fedha. Siwezi kufanya mambo ya aina hiyo.” Amesisitiza Ndung’u.
Kadhalika ametoa wito kwa viongozi wa umma kuhakikisha wanazingatia uadilifu wakati wote, akieleza kuwa kesi za ufisadi mara nyingi huwafuata hata baada ya kuondoka madarakani, bila kujali shinikizo la kisiasa.
“Mikataba hiyo ya ufisadi itakufuata hadi kaburini. Haiendi na serikali au utawala unaokuja baada yako.” Ameongeza.
Ndung’u pia amenukuu ripoti ya Benki ya Dunia iliyochapishwa mwaka 2005, iliyoeleza kuwa nyadhifa za umma nchini Kenya zimekuwa zikitumiwa vibaya kupitia matumizi mabaya ya sheria zilizopo au kutungwa kwa sheria mpya ili kunufaisha watu wenye uhusiano wa kisiasa.
“Kuna chapisho la Benki ya Dunia lililochapishwa mwaka 2005, ambalo lilikuwa na sura maalum kuhusu Kenya kwa sababu kushikilia wadhifa wa umma kulikuwa kumegeuka kuwa rasilimali inayoweza kutumiwa vibaya. Sheria zilizopo zilitumiwa vibaya au sheria mpya kutungwa ili kuelekeza rasilimali kwa watu wa karibu na viongozi.” Ndung’u amebaini.









