Waziri Joho Asimamisha Uchimbaji wa Tata Chemicals Magadi.

0

Waziri wa Madini, Uchumi wa Bluu na Masuala ya Baharini Hassan Ali Joho ameamuru kusimamishwa kwa shughuli za uchimbaji madini za kampuni ya Tata Chemicals Magadi kwa madai ya kutofuata sheria za uchimbaji madini nchini Kenya.

Katika taarifa iliyotolewa Julai 29 2026 Waziri wa Madini, Hassan Ali Joho amesema kampuni hiyo itasalia kufungwa hadi itakapotekeleza kikamilifu matakwa ya Sheria ya Madini, na kanuni nyingine zinazosimamia sekta hiyo.

“Shughuli zimesitishwa hadi kampuni hiyo itakapozingatia kikamilifu Sheria ya Madini, Kanuni zake pamoja na sheria nyingine zote zinazohusika na zinazosimamia sekta ya uchimbaji madini nchini Kenya,” Joho amesema.

Hatua hiyo ni miongoni mwa Misimamo kali zaidi za udhibiti kuwahi kuchukuliwa dhidi ya kampuni kubwa ya uchimbaji madini nchini katika miaka ya hivi karibuni, na inaonyesha dhamira ya serikali ya kuimarisha uzingatiaji wa sheria, kuongeza uwazi katika ukusanyaji wa mapato ya madini, na kuhimiza uchakataji wa madini ndani ya taifa ili kuongeza thamani yake kabla ya kuuzwa.

Joho amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya mazungumzo ya muda mrefu kati ya wizara ya Madini na kampuni hiyo kuhusu wajibu wake wa kisheria chini ya Sheria ya Madini, Kanuni za Leseni na Vibali vya Madini za mwaka 2017 na Kanuni za Ukusanyaji na Usimamizi wa Mrabaha wa Madini za mwaka 2024.

Kampuni hiyo sasa imeagizwa kuwasilisha nyaraka zinazoonyesha imetimiza masharti yote ya kisheria na kushughulikia madeni yote yaliyosalia kabla ya kuruhusiwa kuendelea na shughuli za uchimbaji.

Joho amesema serikali itaendelea kutekeleza sheria katika sekta ya madini ili kuhakikisha kuwa maliasili za nchi zinawanufaisha Wakenya.

“Wizara ya madini inaendelea kujitolea kuhakikisha kuwa rasilimali za madini nchini Kenya zinatumika kwa uwajibikaji na kwa namna inayoiletea taifa manufaa makubwa ya kiuchumi, huku ikilinda mazingira na maslahi ya jamii zinazozunguka maeneo ya uchimbaji madini,” Joho ameongeza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here