Aliyekuwa Waziri wa Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Urithi, Aisha Jumwa Karisa Katana, ametangaza kukigura Chama tawala cha UDA kinachoongozwa na Rais William Ruto, na hivyo kumaliza uhusiano wake na chama tawala.
Akizungumza na wanahabari Alhamisi, Julai 30, 2026 Jumwa amesema ameafikia uamuzi huo baada ya kutafakari kwa kina, kufanya maombi na kushauriana kwa upana na wananchi anaowahudumia.
Jumwa amesema kujiondoa kwake UDA kumeanza kutekelezwa mara moja, akieleza kuwa atatangaza hatua yake inayofuata ya kisiasa hivi karibuni.
“Baada ya kutafakari kwa kina, maombi ya dhati na mashauriano mengi na watu ninaowahudumia, nimefanya mojawapo ya maamuzi magumu zaidi katika maisha yangu ya kisiasa,” amesema Jumwa.
“Kuanzia leo, Aisha Jumwa Katana si mwanachama wa UDA,” ameongeza.
Hata hivyo, Jumwa hajatangaza chama cha kisiasa atakachojiunga nacho, huku wengi wakisubiri hatua yake inayofuata kuelekea msimu wa siasa.
Katika taarifa yake, Jumwa amemshutumu Rais William Ruto kwa kile alichokitaja kama usaliti, akisema licha ya kumuunga mkono kwa muda mrefu katika safari yake ya kisiasa, aliachwa nje ya serikali na kudai kuwa amekuwa akidhalilishwa mara kwa mara.
Jumwa pia amedai kuwa alizuiliwa kuingia katika Ikulu ya Nairobi wakati viongozi kutoka Pwani walikuwa wameenda kukutana na Rais Ruto.
“Huenda hamfahamu, lakini nilifukuzwa kutoka Ikulu wakati viongozi kutoka Pwani walikuja kumwona Rais. Nilikutumia ujumbe, lakini hukuwahi kunijibu. Nimedhalilishwa. Hata unapokuja Kilifi, ni kana kwamba hanitambui tena,” ameongeza.
Ameongeza kuwa licha ya kumuunga mkono Rais Ruto katika nyakati ngumu za safari yake ya kisiasa, hatimaye alihisi kutengwa, huku akimtaka Rais kuheshimu haki zake za kidemokrasia pamoja na za wananchi wa Kilifi.









