Kenya ilitwaa medali yake ya kwanza ya dhahabu katika Michezo ya Jumuiya ya Madola 2026 kwa ushindi wa kihistoria wa mbio za kuruka viunzi na maji Jumatatu tarehe 27 2026.
Kenya ilijinyakulia dhahabu yake kwa ushindi wa kuvutia baada ya Edmund Serem kuongoza ushindi wa kihistoria wa wakenya wote watatu katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji jijini Glasgow, Scotland.
Serem, ambaye ni bingwa wa dunia wa vijana chini ya miaka 20 katika mbio hizo, alishinda kwa muda wa dakika 8:18.23, akifuatwa na mkenya mwenzake Simon Koech aliyetwaa fedha kwa muda wa 8:18.59, huku Leonard Bett akimaliza wa tatu na kujinyakulia shaba kwa muda wa 8:21.63, na hivyo kuifanya Kenya kutwaa nafasi zote jukwaani.
Ushindi huo ulipatikana saa chache baada ya Diana Wanza kuifungulia Kenya kapu la medali za riadha kwa kutwaa fedha katika mbio za wanawake za mita 10,000, na kufikisha jumla ya medali tano: dhahabu moja, fedha mbili na shaba mbili pamoja na iliyonyakuliwa na Joshua Amunga katika uinuaji wa Mizani.
Serem, aliyekuwa na furaha kubwa, alisema ushindi huo ulikuwa ndoto iliyotimia katika ushiriki wake wa kwanza kabisa kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola.
“Nimetwaa taji langu la kwanza katika ushiriki wangu wa kwanza kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola, na nina furaha sana. Najua familia yangu nyumbani ina furaha, na wakenya pia wanafurahia ushindi huu. Zaidi ya yote, tumefanikisha ushindi wa nafasi tatu za juu kwa Kenya.” alisema Serem.
Mwanariadha huyo alikiri kuwa hakutarajia kushinda kutokana na ushindani mkali uliokuwapo, ukiwemo kutoka kwa bingwa wa dunia Geordie Beamish wa New Zealand.
“Sikuwa na uhakika wa kushinda. Washindani walikuwa imara sana. Kulikuwa na bingwa wa dunia Beamish, na pia Simon Koech ambaye hivi karibuni alikimbia chini ya dakika nane. Niliona nina nafasi ya kupanda jukwaani, lakini sikuwa na uhakika wa ushindi hadi mzunguko wa mwisho nilipotambua bado nilikuwa na nguvu za ziada, ndipo nikaongeza kasi,” alisema.
Kwa muda mrefu Kenya imekuwa ikitawala mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji duniani, ikizalisha mabingwa wa Olimpiki na dunia kama Ezekiel Kemboi, Conseslus Kipruto, Brimin Kipruto na Saif Saaeed Shaheen.
Ushindi wa nafasi zote tatu jijini Glasgow uliendelea kuthibitisha hadhi ya Kenya kama taifa linalotawala mbio hizo duniani.
Matokeo hayo pia ni hatua muhimu katika safari ya Serem, ambaye amepanda kwa kasi katika riadha baada ya kutwaa ubingwa wa dunia wa vijana chini ya miaka 20 na kujidhihirisha kama mmoja wa wanariadha chipukizi wenye matumaini makubwa nchini Kenya.
Huku mashindano ya riadha yakizidi kushika kasi katika michezo hiyo, ni matarajio ya kikosi cha Kenya kwamba ushindi huo ungewapa hamasa wanariadha wengine kuongeza idadi ya medali kadri mashindano yanavyoendelea jijini Glasgow.









