NCIC Yaanzisha Uchunguzi Dhidi Ya Viongozi Watatu Wakuu.

0

Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) imeanzisha uchunguzi dhidi ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Waziri wa Afya Aden Duale na Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku kwa madai ya kutoa matamshi ya chuki na uchochezi.

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa mnamo tarehe 28 Julai 2026, kwa ushirikiano na Baraza la Dini Nchini (Interreligious Council of Kenya), NCIC pia imesema inawachunguza Gavana wa Busia Paul Nyongesa Otuoma, Naibu Gavana wa Mandera Ali Maalim Mohamud, Mbunge wa Sirisia John Waluke, Mbunge wa Kipipiri Wanjiku Muhia na Mbunge wa Nakuru Mashariki David Gikaria.

Mwenyekiti wa NCIC, Kasisi Dkt. Kepha Omae, amesema uchunguzi huo unafanyika kwa mujibu wa sheria na kwamba wote wanaochunguzwa wana haki ya kufuata mchakato wa kisheria hadi pale watakapopatikana na hatia.

“Uchunguzi huu unaendelea kufanywa kwa kuzingatia sheria kikamilifu. Tunawahakikishia kwamba watu wote wanaochunguzwa wataendelea kufurahia haki zao zote za kikatiba hadi pale watakapothibitishwa kuwa na hatia na mahakama,” amesema Omae.

Aidha, tume hiyo imewataja Tipape Naini Musa na Dkt. Dennis Ouma kuwa miongoni mwa wanaochunguzwa, ikisisitiza kuwa haitayumbishwa na nyadhifa au ushawishi wa mtu yeyote anayehusishwa na uchunguzi huo.

Omae amesema NCIC itashirikiana kwa karibu na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi (EACC), Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP), Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) pamoja na mashirika mengine ya uchunguzi ili kuhakikisha yeyote atakayepatikana na makosa anachukuliwa hatua za kisheria.

Akijibu wito wa baadhi ya Wakenya waliotaka tume hiyo itumie video fupi zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kama ushahidi, Omae amesema NCIC hufuata taratibu za kisheria na haiwezi kuanzisha uchunguzi kwa kutegemea video za mitandao ya kijamii pekee.

Amewataka wananchi kuwasilisha malalamishi rasmi au maombi kwa tume ili kurahisisha uchunguzi.

“Sisi ni taasisi inayozingatia utaratibu wa kisheria. Hatuwezi kuchukua hatua kwa kutegemea video fupi zinazosambazwa kwenye TikTok pekee. Tunawahimiza wananchi kuripoti kwetu matukio ya uchochezi ili yafanyiwe uchunguzi,” ameongeza Omae.

Hatua hiyo inajiri siku moja baada ya Waziri wa Ardhi Alice Wahome kumkosoa Waziri wa Afya Aden Duale kutokana na matamshi yake yaliyotafsiriwa kuwa ya kikabila.

Wahome alimtaka Duale kuyafuta matamshi hayo na kuomba radhi bila masharti, akisisitiza kuwa kauli za viongozi wengine zilizowahi kutolewa hazipaswi kutumika kuhalalisha matamshi yake.

“Makosa mawili hayasahihishi jambo, na ni mpumbavu pekee asiyebadili msimamo wake anapogundua amekosea,” aliandika Wahome.

Kwa upande wake, Duale alisisitiza kuwa hataomba msamaha, akitaka NCIC pia imchunguze Rigathi Gachagua kwa kile alichodai ni matamshi ya mara kwa mara yanayochochea ukabila kabla ya kumhoji yeye.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here