“Fire Man” Kindiki Apuuza Tetesi Za Kupunguziwa Moto.

0

Naibu wa Rais Professa Kithure KIndiki amepuuza tetesi kuwa amepokonywa jukumu muhimu la kuratibu ushirikiano wa serikali kuu na za kaunti katika kutoa huduma, kutekeleza sera mbalimbali na kufanikisha majukumu ya Pamoja.

Kwenye kurasa zake za kijamii ameandika kuwa taarifa hizo ni potovu akirejelea tetesi zilizoenea kiasi cha kuwa kwenye ukurasa wa mbele wa Gazeti moja humu nchini Jumanne Tarehe 27 Julai 2026.

“Habari Potovu” ameandika Kindiki.

Kwa kawaida jukumu hilo limekuwa likitekelezwa na Afisi ya Naibu wa Rais.

Jukumu hilo limemfanya kuhudumu katika nafasi ya Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Bajeti na Uchumi IBEC linaloshirikisha serikali hizo mbili katika kujadili ugavi wa rasilmalli, mipango ya bajeti na maswala mengine ya maendeleo.

Hata hivyo Ripoti zimeenea kwamba Rais William Ruto kupitia Afisi ya Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei amemwagiza Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi kuchukua jukumu hilo.

Sababu kuu zilizoorodheshwa ni kwamba Kindiki ana majukumu mengi na hivyo ni bora kumpunguzia baadhi.

Aidha Nyaraka zilizosambazwa zinaeleza kuwa kifungu cha 147 Ibara ya 4 ya Katiba hakimruhusu Naibu wa Rais kutekeleza majukumu yaliyotengewa afisi ya Waziri.

Kulingana na sheria iliyoandaliwa na Mwanasheria mkuu Dorcas Oduor ya ushirikiano wa serikali kuu na zile za kaunti mapema mwaka huu, jukumu la kusimamia sheria hiyo lilistahili kuwa chini ya Waziri wala si Naibu wa Rais.

Hata hivyo gumzo limeendelea licha ya KIndiki kupuzilia mbali tetesi hizo za kupokonywa jukumu hilo baadhi wanahisi nafasi yake iko kwenye hatari kubwa kuelekea uchaguzi mkuu ujao 2027 huku nafasi ya Mgombea mwenza iking’ang’aniwa na viongozi mbalimbali nje ya Eneo la Mlima Kenya Hususan chama cha ODM.

“Iwapo UDA itatoa mgombea wa urais, basi ODM lazima itoe mgombea mwenza wa urais. Huo ndio msimamo wetu kama ODM.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here