Profesa John Okumu ameteuliwa kuwa makamu chanzela wa saba wa chuo kikuu cha Kenyatta.
Uteuzi wake uliotangazwa Jumatatu tarehe 27 Julai 2026 ulifuatia mchakato wa ushindani ulioendeshwa na Tume ya Utumishi wa Umma (PSC), ambapo aliibuka bora, kwa mujibu wa mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Kenyatta, Profesa Clara Momanyi.
Profesa Okumu aliwahi kuhudumu kama naibu makamu chanzela wa chuo (masuala ya taaluma) kwa kipindi cha miaka kumi, pamoja na kushikilia nyadhifa mbalimbali za juu za usimamizi katika chuo hicho.
“Yeye ni msomi na msimamizi mwenye uzoefu mkubwa anayekuja na hazina ya uzoefu katika uongozi wa kitaaluma, utafiti na maendeleo ya taasisi,” Profesa Momanyi alisema katika taarifa.
“Kwa kuzingatia uzoefu wake wa kina na uelewa wa kimkakati katika usimamizi wa elimu ya juu, upangaji wa kimkakati na ushirikiano na wadau, Baraza la Chuo lina imani kwamba atatoa uongozi wa maono na wa mageuzi utakaoongoza chuo katika hatua yake inayofuata ya ukuaji na ubora.”
Akizungumza baada ya uteuzi huo, Profesa Okumu alilishukuru baraza la chuo kwa kumwamini na kumpa jukumu hilo, huku akiahidi kuiongoza taasisi hiyo kupitia mbinu shirikishi na ya kuleta mageuzi.
“Nimeheshimika sana kwa imani ambayo baraza la chuo limeweka kwangu. Nimejitolea kuongoza kwa unyenyekevu, uadilifu na uwazi tunaposhirikiana kuimarisha nafasi ya Chuo Kikuu cha Kenyatta kama chuo kikuu kinachoongoza nchini Kenya na taasisi yenye ushindani wa kimataifa,” alisema.
Aidha, aliahidi kutetea na kuendeleza elimu bora huku akifanya kazi kwa ushirikiano na wafanyakazi, wanafunzi na wadau wengine ili kuendeleza dhamira ya chuo ya kutoa elimu, utafiti na huduma za kiwango cha juu.
Profesa Okumu anaingia madarakani kujaza nafasi iliyoachwa wazi kufuatia kustaafu kwa mtangulizi wake, Profesa Paul Wainaina, mnamo Januari 2026.
Okumu alipata shahada yake ya Elimu (Sayansi) mwaka 1986 katika chuo hicho, akibobea katika Fizikia katika shahada ya kwanza.
Baadaye alipata Shahada ya Uzamili (MSc) ya Fizikia (Condensed Matter Physics) mwaka 1988, pia katika chuo hicho.
Mwaka 1996 alipata Shahada ya Uzamivu (PhD) katika ulingo huo huo kutoka Chuo Kikuu cha Leeds nchini Uingereza.
Alipanda ngazi za taaluma kutoka nafasi ya mhadhiri msaidizi mwaka 1988 hadi kuwa profesa mshiriki mwaka 2004 katika chuo kikuu cha Kenyatta.
Profesa Okumu pia ametoa mchango mkubwa katika tafiti za kitaaluma, ikiwa ni pamoja na kuchapisha makala 26 katika majarida ya kimataifa yaliyopitiwa na wataalamu, makala 18 katika machapisho ya makongamano ya kisayansi, na ameandika vitabu kadhaa.
Aidha, yeye ni mwanachama wa mtandao wa taasisi ya Alexander von Humboldt, unaosaidia mafunzo ya wanasayansi chipukizi wa Afrika na kubadilishana taarifa za kisayansi.









