Starlets wapoteza Nyota ya ufunguzi WAFCON

0

Safari ya Harambee Starlets kurejea kwenye jukwaa kubwa la soka la wanawake barani Afrika baada ya kusubiri kwa miaka kumi ilianza kwa matokeo mabaya usiku wa Jumapili tarehe 26 Julai, baada ya wenyeji Morocco kuifunga mabao 4-0 katika mechi ya ufunguzi ya Kundi A ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026, jijini Rabat.

Mbele ya maelfu ya mashabiki wa nyumbani waliokuwa wamefurika uwanja wa Moulay El Hassan, Morocco (Atlas Lionesses) walitawala mchezo tangu dakika za mwanzo na kuwapa wabinti wa Kenya somo kali katika mechi yao ya kwanza ya kurejea kwenye mashindano hayo.

Mchezo ungeweza kuwa na mwelekeo tofauti kabisa kama Kenya ingetumia nafasi ya mapema ya kufunga katika dakika za mwanzo za kipindi cha kwanza, ambapo mshambuliaji Tereza Engesha alipata nafasi nzuri ya kuipa Starlets bao la kuongoza, lakini shuti lake kali liligonga mwamba wa goli na kutoka nje.

Morocco walitumia vyema nafasi hiyo iliyopotezwa na Kenya na kufungua ukurasa wa mabao katika dakika ya 20 kupitia kwa Sakina Ouzraoui, aliyemalizia kwa ustadi.

Kabla kikosi cha kocha Beldine Odemba hakijajipanga upya, Atlas Lionesses waliongeza mabao mawili kwa haraka, Maryme Atiq alifunga bao la pili katika dakika ya 29, na dakika mbili baadaye mkongwe mwenye umri wa miaka 33, Jraidi, aliruka juu ya mabeki wa Kenya na kufunga kwa kichwa, huku kipa Lilian Awuor akiwa hana nafasi ya kuokoa mpira.

Wakati wa kipenga cha mapumziko, Harambee Starlets walikuwa nyuma kwa mabao 3-0 baada ya kipindi cha kwanza kilichoonekana kuwa kigumu kwao.

Akitafuta mabadiliko, kocha mkuu Beldine Odemba alifanya mabadiliko matatu wakati wa mapumziko, akiwaingiza Shilwatso na Shirleen Opisa ili kuimarisha safu ya ushambuliaji na kurejesha matumaini ya timu.

Hata hivyo, matumaini yoyote ya kurejea mchezoni yalizimwa mapema kipindi cha pili kilipoanza ambapo dakika mbili tu baada ya mchezo kuanza tena, Jraidi alifunga bao lake la pili na kuongeza uongozi wa Morocco kuwa mabao 4-0.

Zikiwa zimesalia dakika 30 mchezo kumalizika, Kenya ilianza kucheza vizuri zaidi, ikimiliki mpira kwa vipindi virefu na kuisukuma Morocco kujilinda katika eneo lao kwa muda wote uliosalia ila hilo halikuwanyima wenyeji pointi zote tatu.

Sasa Kenya italazimika kujipanga upya kabla ya kuivaa Senegal Julai 30, ambapo matokeo mazuri pekee ndiyo yatakayodumisha matumaini yao ya kufuzu hatua ya mchujo na kuendeleza ndoto ya kufuzu Kombe la Dunia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here