Mamlaka ya kitaifa ya uchukuzi na usalama barabarani NTSA imetoa onyo kali kwa Madereva na wamiliki wa magari ikiwataka kuhakikisha kuwa magari yao yako katika hali nzuri na yana leseni halali kabla ya kuanza safari huku wanafunzi wakianza likizo ya Agosti.
Katika taarifa yake Julai 27 2026, NTSA imesema madereva na wamiliki wa magari wana jukumu la kuhakikisha magari yanayotumika barabarani yanakidhi viwango vya usalama ili kulinda maisha ya wanafunzi na watumizi wengine wa Barabara.
“Madereva na wamiliki wa magari wana wajibu wa kuhakikisha magari yao yako katika hali nzuri ya matumizi na yana leseni halali, huku shule zikijiandaa kufungwa kwa likizo,” NTSA imesema.
Onyo hilo linajiri wakati maelfu ya wanafunzi wanatarajiwa kusafiri kuelekea nyumbani kwa likizo ya Agosti hatua itakayoongeza idadi ya mabasi ya shule, matatu na magari binafsi barabarani.
“Huku shule mbalimbali nchini zikijiandaa kufungwa kwa likizo ya mwezi Agosti, NTSA inawakumbusha watumiaji wote wa Barabara hasa wanaotoa huduma za usafiri kuweka usalama wa watoto mbele.” NTSA imeongeza.
NTSA imesema itaimarisha ukaguzi wa magari wanaosafirisha wanafunzi kwa kushirikiana na Idara ya kitaifa ya polisi NPS Pamoja na Kamati za Kaunti za uchukuzi na usalama.
Ukaguzi huo utalenga kubainisha hali ya magari. Matumizi ya vifaa vya kudhibiti mwendo, mikanda ya usalama, magurudumu, breki na mahitaji mengine muhimu ya usalama.
Aidha Mamlaka hiyo imeonya kuwa itachukua hatua kali dhidi ya madereva watakaopaikana wakiendesha magari yao kwa kasi, kuwabeba abiria kupita kasi, kuendesha magari wakiwa wamelewa chakari vitendo vinavyotajwa kuwa miongoni mwa sababu kuu za Ajali mbaya za barabarani.









