Wakenya wote watakaohitaji matibabu ya dharura watapata huduma chini ya mpango wa dharura wa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), bila kujali kama wamejisajili katika mpango wa bima ya afya ya taifa au la.
Rais William Ruto ametangaza hatua hiyo inayolenga kuhakikisha kwamba hakuna mkenya atakayenyimwa huduma ya kuokoa maisha kwa sababu ya kukosa bima ya afya au uwezo wa kugharamia matibabu.
Akizungumza Alhamisi tarehe 5 Agosti wakati wa uzinduzi wa huduma ya dharura ya matibabu ya SHA na kituo cha kitaifa cha kuratibu na kutuma ambulensi jijini Nairobi, rais Ruto alisema mpango huo unaashiria mabadiliko makubwa katika mfumo wa afya nchini kwa kuhakikisha huduma za dharura zinatolewa kama haki ya kikatiba badala ya kutegemea uwezo wa kifedha wa mgonjwa.
“Ulinzi huu unawahusu wagonjwa wote, wawe wamejisajili na SHA au la,” alisema rais Ruto.
Alisema huduma ya usafirishaji wa wagonjwa kwa ambulensi pamoja na saa 24 za kwanza za matibabu ya dharura zitafadhiliwa kupitia hazina ya dharura, ya magonjwa sugu kwa viwango vilivyoidhinishwa.
Kwa mujibu wa rais, wagonjwa waliohitaji matibabu ya haraka hawatalazimika tena kuwasilisha uthibitisho wa bima au kufanya malipo kabla ya kupokea huduma.
“Hakutakuwa na mazungumzo, dhamana wala ndugu kukimbizana kutafuta fedha. Katika hali ya dharura, swali la kwanza halipaswi kuwa kama mgonjwa ana uwezo wa kulipa. Wajibu wa kwanza ni kuokoa maisha,” alisema rais.
Kiongozi wa taifa alisema mageuzi hayo yanaanzisha mfumo wa kitaifa wa huduma za dharura unaowalinda wakenya wote bila kujali hali yao ya usajili chini ya SHA.
Kama sehemu ya mageuzi hayo, serikali imetoa nambari moja ya kitaifa ya huduma za dharura, 922, ambayo itapatikana bila malipo kupitia mitandao yote.
Kila simu ya dharura itakayopigwa itapokelewa na maafisa waliopata mafunzo maalumu, ambao watatambua na kutuma ambulensi iliyo karibu zaidi, kisha kumwelekeza mgonjwa katika kituo cha afya chenye uwezo bora wa kushughulikia hali yake.
“Lengo si kumpeleka mgonjwa katika hospitali iliyo karibu zaidi, bali katika hospitali yenye uwezo mkubwa zaidi wa kuokoa maisha yake,” alisema.
Aliagiza vituo vyote vya afya vilivyo na mikataba chini ya SHA kutowanyima, kutowachelewesha, kutowarejelea au kuwahamisha wagonjwa wanaohitaji matibabu ya dharura kwa sababu hawawezi kulipa au kwa kuwa taarifa zao za bima hazijathibitishwa.
Aidha, Ruto alizitaka serikali za kaunti, mashirika ya kidini na waendeshaji binafsi wa huduma za ambulensi kushirikiana na serikali katika kupanua huduma za dharura kote nchini.
Alisema zaidi ya watoa huduma 1,243 wa ambulansi na huduma za dharura tayari wameingia kwenye mikataba chini ya SHA, lakini akaiagiza wizara ya Afya, SHA na baraza la magavana kuhakikisha kila mtoa huduma anayekidhi vigezo kutoka sekta za umma, kaunti, mashirika ya kidini na sekta binafsi anaunganishwa katika mfumo wa kitaifa wa uratibu wa huduma za dharura kufikia tarehe 30 Desemba mwaka 2026.









