Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli amesema Huduma ya Kitaifa ya Polisi itaendelea kutekeleza sheria kwa haki na bila ubaguzi, akisisitiza kuwa Wakenya wote ni sawa mbele ya sheria.
Akizungumza baada ya kufunga rasmi kambi ya Mashindano ya Kitaifa ya Skauti nchini mjini Thika, Masengeli amepuuza madai kwamba polisi huchagua watu wa kuwachukulia hatua za kisheria, hususan viongozi wa kisiasa wanaoshukiwa kutoa matamshi ya uchochezi.
“Sheria ni kama kioo; inamhusu kila mtu bila kujali wewe ni nani. Kila mmoja anapaswa kuitii na kuzingatia utawala wa sheria,” amesema Masengeli.
Aidha, amesisitiza kuwa shughuli za Huduma ya Kitaifa ya Polisi zinaongozwa na Katiba na sheria za nchi, na kwamba hakuna mtu aliye juu ya sheria.
“Kila mtu ana haki zake, lakini haki ya mtu mmoja haiondoi wala kusimamisha haki za wengine. Ndiyo maana kila mmoja anapaswa kutekeleza haki zake kwa kuzingatia sheria na kuheshimu haki za wengine,” ameongeza Masengeli.
Aidha, ameahidi kuwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi itaendelea kukabiliana vikali na magenge ya uhalifu pamoja na watu wanaohusika na vitendo vya vurugu.
“Hatutaruhusu kabisa vitendo vya kihuni. Wahuni wote watakabiliwa vikali na sheria.”
“Ni wakati wa kubadilika; wale waliokuwa wanategemea biashara za kihuni wanapaswa kubadilika na kufanya shughuli nyingine halali. Wanapaswa kuwa watu wema na kuiga mfano wa Skauti wa Kenya,” amesisitiza Masengeli.
Kadhalika amewataka vijana wanaoshiriki katika vurugu wakati wa mikutano ya kisiasa kukoma na badala yake kujikita katika shughuli zenye manufaa.
Amewahimiza vijana hao kujiunga na vuguvugu la Skauti, akisema linajenga nidhamu, uzalendo, uongozi na kuwajibika kwa taifa.
Kauli ya Masengeli inajiri wakati kukiwa na mjadala mkubwa kuhusu kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa viongozi wa kisiasa wanaodaiwa kutoa matamshi ya uchochezi, huku baadhi ya watu wakiibua wasiwasi kuhusu matumizi sawa ya sheria kwa wote.









