Wito wa “Wantam” Unasukumwa na Chuki na Ukabila.

0

Waziri wa Afya Aden Duale amewashutumu viongozi wanaopendekeza Rais William Ruto kuhudumu kwa muhula mmoja pekee, akidai msimamo huo unasukumwa na ukabila, chuki na maslahi binafsi.

Akizungumza katika Ikulu ya Nairobi wakati wa mkutano wa Rais Ruto na viongozi wa dini ya Kiislamu, Duale amepuuzilia mbali wito huo, akisema haujengwi kutokana na ajenda ya kweli ya maendeleo ya taifa.

Duale amesema mjadala kuhusu uongozi wa nchi unapaswa kuzingatia sera na maslahi ya Wakenya badala ya misingi ya chuki au migawanyiko ya kisiasa.

“Kwa sababu ya ukabila, ubinafsi na chuki, unasikia baadhi ya watu wakisema Ruto anapaswa kuhudumu kwa muhula mmoja,” amesema Duale.

Duale amesisitiza kuwa utendakazi wa serikali unapaswa kupimwa kwa kuzingatia mipango yake ya maendeleo na juhudi za kuhakikisha ushirikishwaji wa kila mmoja.

“Kenya ni yetu sote,” amesema Duale.

Duale pia amerejelea historia ya marais waliotangulia humu nchini akimtetea Rais William Ruto kuhudumu kwa muhula wa pili.

Amesema Rais wa kwanza wa Kenya Jomo Kenyatta alihudumu kwa miaka 15, aliyemrithi Daniel arap Moi akiongoza kwa miaka 24, huku Mwai Kibaki akiwa madarakani kwa miaka 10 na Uhuru Kenyatta pia akihudumu kwa mihula miwili iliyokamilika kwa miaka 10.

“Asubuhi inapofika, huwezi kuificha kwa kiganja chako,” ameongeza Duale.

Aidha, ametetea rekodi ya serikali ya Rais Ruto, akitaja ongezeko la ushirikishwaji wa kila Mkenya serikalini, ugavi sawa wa rasilimali za maendeleo pamoja na miradi ya miundombinu inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema mbinu ya serikali inalenga kuhakikisha kila Mkenya anahisi kuwa sehemu ya utawala bila kujali eneo analotoka.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here