Tunataka Ukweli Kuhusu Kifo cha Erick Otieno Kizuizini Faith Odhiambo Ashurutisha NPS.

0

Aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Nchini (LSK), Faith Odhiambo, ameitaka Mamlaka Huru ya Kuangazia Utendakazi wa Maafisa wa Polisi IPOA kufanya uchunguzi wa haraka na wa kina kuhusu kifo cha mwendesha bodaboda mwenye umri wa miaka 19, kwa jina Erick Otieno, aliyefariki akiwa kizuizini katika Kituo cha Polisi cha Muthaiga.

Odhiambo amesema mazingira ya kifo cha Otieno yanaibua maswali mazito na yanafanana na yale ya mwanablogu Albert Ojwang, aliyefariki akiwa mikononi mwa polisi mwaka 2025.

Akizungumza baada ya kukutana na familia ya marehemu, Odhiambo amesema Erick Otieno alifariki usiku wa Jumapili akiwa amezuiliwa katika kituo hicho cha polisi, huku akidai kuwa hadi sasa polisi hawajatoa maelezo ya kuridhisha kuhusu mazingira ya kukamatwa kwake na kilichotokea akiwa mhabusu.

Kwa mujibu wa Odhiambo, ripoti ya uchunguzi wa maiti imeonyesha kuwa Otieno alipata majeraha mengi yaliyotokana na kupigwa kwa kifaa butu, hasa katika sehemu ya kifua na tumbo.

Aidha, ameitaka IPOA pamoja na Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu (KNCHR) kuhakikisha ushahidi wote muhimu unalindwa.

“Tunataka picha za kamera za CCTV za Kituo cha Polisi cha Muthaiga zichukuliwe mara moja na Mamlaka Huru ya Kuangazia Utendakazi wa Maafisa wa Polisi (IPOA) pamoja na Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu (KNCHR), ili kuhakikisha ushahidi huo hauhitilafiwi na pia tunataka rekodi kamili itolewe,” amesema Odhiambo.

Kauli hiyo inajiri wakati IPOA tayari imeanzisha uchunguzi kuhusu kifo hicho.

IPOA imethibitisha kuwa imepokea ripoti ya uchunguzi wa maiti pamoja na taarifa kutoka kwa familia ya marehemu, huku uchunguzi ukiendelea kubaini mazingira yaliyosababisha kifo cha Erick Otieno.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here