Anapohitimisha kipindi chake cha miaka miwili na miezi kumi kama Msemaji wa Serikali, Dkt. Isaac Mwaura ametaja wizara, idara za serikali na mashirika ya umma yaliyofanya vizuri zaidi katika mawasiliano na ushirikishwaji wa wananchi.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya ofisi, Dkt. Mwaura amesema mawasiliano ya kimkakati ni nguzo muhimu ya utawala bora kwa kuwa hujenga imani ya wananchi, hufafanua sera za serikali na kuwawezesha wananchi kuelewa athari za mipango mbalimbali ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Dkt. Mwaura, Wizara ya Fedha ndiyo inayoongoza kwa mawasiliano bora.
Amempongeza Waziri wa Fedha John Mbadi kwa uwezo wake wa kueleza masuala tata ya uchumi, bajeti na sera za kifedha kwa lugha rahisi inayoweza kueleweka na wananchi wa kawaida.
Amesema wizara hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu hatua za kufufua uchumi, usimamizi wa deni la taifa na sera za ushuru.
“Wizara ya Hazina imeonyesha kuwa hata masuala magumu ya uchumi yanaweza kuelezwa kwa njia ambayo wananchi wanaweza kuyaelewa bila kupoteza usahihi wa taarifa,” amesema Dkt. Mwaura.
Nafasi ya pili imechukuliwa na Wizara ya Afya, ambayo ameisifu kwa kuendelea kuwapa wananchi taarifa kuhusu mageuzi ya sekta ya afya licha ya changamoto zilizopo, ikiwemo ufadhili wa huduma za afya, milipuko ya magonjwa na utekelezaji wa mageuzi ya mfumo wa afya.
“Wizara ya Afya chini ya uongozi wa Waziri Aden Duale imefanya kazi kubwa licha ya mazingira magumu na changamoto nyingi zilizokabili sekta hiyo.” Ameeleza Mwaura.
Wizara ya Kilimo nayo imeshika nafasi ya tatu kutokana na mawasiliano yake kuhusu ruzuku ya mbolea, usalama wa chakula, miradi ya umwagiliaji na programu za kuwasaidia wakulima.
Katika idara za serikali, Dkt. Mwaura ameiorodhesha Idara ya Usalama wa Ndani kama iliyofanya vizuri zaidi, akimpongeza katibu katika idara ya usalama Dkt. Raymond Omollo kwa kutoa taarifa kwa wakati kuhusu masuala ya usalama, majanga na shughuli za serikali.
Pia ameipongeza Idara ya Makazi na Maendeleo ya Miji chini ya katibu Charles Hinga kwa mawasiliano kuhusu Ujenzi wa nyumba za bei nafuu, pamoja na Idara ya Afya ya Umma inayoongozwa na Mary Muthoni kwa kampeni zake za kuhamasisha afya na kuzuia magonjwa.
Aidha, Idara ya Masuala ya kigeni inayosimamiwa na Katibu Roseline Njogu imepongezwa kwa mawasiliano yake na Wakenya wanaoishi ughaibuni.
“Idara ya Usalama na Maswala ya Ndani, Idara ya Makazi na Maendeleo ya Miji, Idara ya Afya ya Umma na Idara ya Masuala ya Kigeni ndizo bora katika kutoa mawasiliano na zinastahili kutambuliwa na kupongezwa kwa mchango wao.” Mwaura ameongeza.
Kwa upande wa mashirika ya serikali, Dkt. Mwaura ameitaja Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu nchini, KeNHA kama shirika lililobobea kwenye utoaji wa taarifa kuhusu miradi ya barabara na hali ya usafiri, huku Mamlaka ya Bandari Nchini (KPA) ikishika nafasi ya pili kwa mawasiliano kuhusu shughuli za Bandari ya Mombasa na maendeleo ya biashara.
Aidha Mwaura ameipongeza Tume ya Kitaifa ya Jinsia na Usawa (NGEC) kwa mawasiliano yake kuhusu usawa wa kijinsia, ujumuishaji wa makundi maalum na ulinzi wa watu walio katika mazingira hatarishi.
Akihitimisha kipindi chake ofisini, Dkt. Mwaura amesema mawasiliano ya serikali hayapaswi kuwa ya kujibu tu hoja zinapozuka, bali yanapaswa kueleza sera kwa uwazi, kupambana na taarifa potofu na kuwapa wananchi taarifa sahihi kwa wakati.
Amesisitiza kuwa mawasiliano bora husaidia kuziba pengo kati ya sera za serikali na uelewa wa wananchi, hivyo kuimarisha uwajibikaji na kuongeza imani ya umma kwa taasisi za serikali.
Aidha, ametoa wito kwa taasisi zote za umma kuendelea kutumia mawasiliano kama nyenzo ya uwazi, ushirikishwaji wa wananchi na kuimarisha mshikamano wa kitaifa, akisisitiza kuwa wananchi wenye taarifa sahihi ni msingi muhimu wa demokrasia na maendeleo ya nchi.









