Miaka 16 ya Katiba, Msemaji wa Serikali Charles Owino Asema Serikali Imezingatia Katiba.

0

Msemaji wa Serikali Charles Owino ametetea rekodi ya serikali katika kulinda haki za kibinadamu, akiwataka wakosoaji wa serikali na vyombo vya habari kuchunguza sera za serikali kwa haki na kwa kuzingatia ukweli na takwimu.

Akizungumza na wanahabari wakati Kenya inapoadhimisha miaka 16 tangu kuzinduliwa kwa Katiba ya 2010, Owino amesema demokrasia inahitaji kuwepo kwa serikali na upinzani, huku pande zote zikitoa misimamo yao kwa kuzingatia ukweli.

“Ni lazima tuulizane maswali magumu, serikali na upinzani, kwa sababu hii ni demokrasia. Lazima kila wakati tuwe na serikali na pia upinzani. Lazima tueleze hisia na misimamo yetu kwa kuzingatia ukweli na takwimu,” amesema Owino.

Owino pia ametetea namna polisi wanavyoshughulikia maandamano, akisema Katiba inalinda haki ya wananchi kufanya maandamano ya amani, lakini polisi wana wajibu wa kuingilia kati pale maandamano yanapogeuka kuwa ya vurugu au kusababisha uharibifu wa mali.

“Tunapowaruhusu watu kufanya maandamano ya amani kama ilivyo katika Katiba, watu wanaishia kuchoma matairi barabarani,” amesema Owino.

Amesema hatua za kiusalama huwa muhimu pale maandamano yanapohatarisha usalama wa umma au kuvuruga amani.

Kadhalika Owino amewataka viongozi wa upinzani kueleza mipango yao kwa Wakenya badala ya kuangazia tu suala la kuiondoa serikali iliyoko madarakani.

“Rais lazima aondoke. Tunajua Rais lazima aondoke wakati fulani. Iwe muhula mmoja au miwili, lazima aondoke kwa sababu Katiba yetu imeeleza hivyo. Lakini mnaacha nini kwa vijana hawa wanaokuja? Mtafanya nini vizuri zaidi?” ameuliza Owino.

Amesema viongozi wa kisiasa wanapaswa kuwasilisha sera na mipango madhubuti itakayoboresha maisha ya Wakenya.

Kauli ya Owino inajiri Kenya inapoadhimisha miaka 16 tangu kupitishwa kwa Katiba ya 2010, ambayo imeleta mabadiliko makubwa katika mfumo wa utawala, ikiwemo kuanzishwa kwa serikali za kaunti, kuimarishwa kwa taasisi huru na kupanuliwa kwa ulinzi wa haki na uhuru wa kimsingi wa raia.

Rais William Ruto alitangaza Agosti 27 kila mwaka, kuwa siku ya kitaifa ya Katiba ikiwa ni siku ya Wakenya kutafakari safari ya demokrasia na maendeleo yaliyopatikana tangu kupitishwa kwa Katiba hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here